0


Displaying IMG_2835.JPGSerikali haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini bali imechukua hatua ya kudhibiti matumizi ya fedha hizo ili kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (MB) alipokutana na wawakilishi wa wafanyabiashara mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya  biashara nchini. 

Amesema kuwa sheria haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini lakini inasisitiza kuwa watu wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya nchi.

“Tatizo kubwa tunalokumbana nalo ni uhuru ulioachiwa ambao unasababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu kwani kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni pia watumiaji wa fedha za kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko sokoni kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti cha thamani ya kubadili fedha za kigeni”. alifafanua Dkt. Kijaji.

Ili kuondoa changamoto hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu huku ambayo inazitaka  bei zote hapa nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki. 

“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Hata hivyo kama mlengwa akitaka kulipa kwa Shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni” alieleza Dkt. Kijaji.

Aidha, viwango vya kubadilishia fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu nyingine vimetakiwa kuwekwa wazi na visizidi vile vya sokoni. 

Mkazi yeyote wa Tanzania au mtu wa nje anayeishi Tanzania  asilazimishwe kufanya malipo yoyote kwa kutumia fedha za kigeni kama ana Shilingi ya Tanzania mkononi mfano gharama za shule na hoteli.

Aidha Serikali imeagiza vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa na Serikali.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji alitoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuhimiza matumizi ya sarafu ili kuweza kukuza thamani ya Shilingi hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top