Mmiliki
wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah, ametoweka kwa zaidi ya wiki
moja sasa na gari lake aina ya Toyota Landcruizer kukutwa likiwa
limeteketea kwa moto katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Gari
hilo lililokuwa likitumiwa na mfanyabishara huyo ambaye ni mkazi wa
Mwanza, lilikutwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara jana
likiwa limeteketea kwa moto.
Ofisa
Habari wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustapher Mwalongo,
amesema kuwa mfanyabishara huyo licha ya gari lake kukutwa limeteketea
kwa moto, hawakukuta mabaki ya mwili wake.
"Gari
lake limeteketea kweli lakini hatujabaini kama na yeye alikuwa kwenye
gari lile kwa sababu waliofika eneo la tukio hawajakuta mwili au mabaki
ya aina yoyote," alisema Mwalongo.
Alisema
baada ya mmiliki huyo wa mabasi kutoweka tangu Machi mosi, kamati
iliundwa ya kufuatilia sababu za kutoweka kwake na wapi alipo ambayo
inashirikiana na familia.
"Kamati
ilipopata taarifa kuwa kuna gari limeteketea kule Serengeti,
walishirikiana na Jeshi la Polisi kwenda hadi eneo la tukio na kubaini
kweli ni lake lakini ndani hawajabaini kama alikuwemo mle wakati
linachomwa," alisema Mwalongo.
Alisema
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku kamati hiyo ikiendelea na
jitihada mbalimbali za kumsaka na kwamba hakuna uthibitisho wa aina
yoyote ya kuwa amefariki dunia akiwa ndani ya gari lililoungua.
"Hakuna
taarifa rasmi za mfanyabishara huyo kufa licha ya baadhi ya mitandao ya
kijamii kuandika kuwa amefariki dunia. Hakuna mwili uliokutwa katika
eneo lile," alisema.
Alisema wawakilishi wa Taboa mkoani Mwanza wanafuatilia kwa karibu na kuwapa kila taarifa wanayoipata kuhusiana na tukio hilo.
Pia
alisema hadi jana jioni kamati hiyo kwa kushiriana na askari wa
wanyamapori walikuwa wanaendelea kumsaka mfanyabishara huyo katika
hifadhi hiyo.
Kuhusu
kutoweka kwake, Mwalongo alisema mara ya mwisho walikutana kwenye kikao
cha kamati ndogo ya Taboa mkoani Mwanza Februari 26, mwaka huu.
Alisema kuanzia Machi mosi zilianza kuzuka taarifa za kutopatikana kupitia simu zake za mkononi hadi nyumbani kwake.
Mabasi ya Kampuni ya Super Sami yanafanya safari zake kati ya Mwanza na mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Kagera.
Post a Comment
karibu kwa maoni