ZAIDI
ya wakazi elfu 30 wa kata mbili za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa
mkoani Dodoma wanatarajia kuondokana na adha ya kukosa huduma ya afya
karibu na maeneo yao baada ya Serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni
mia 6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kitakachengwa katika
kitongoji cha Itongwi, kijiji cha Kalamba kata ya Kalamba.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, ametembelea eneo hilo na
kushuhudia wananchi wenye ari wakiwa wamejitolea nguvu zao kusafisha
eneo ambalo kituo hiko kitajengwa ili kuwaondolea adha ya muda mrefu ya
kufuata huduma za afya Kondoa mjini umbali wa zaidi ya kilometa 100.
Wakazi
wa Kata za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa mkoani Dodoma walijitokeza
wakiwa na majembe, miundu, mapanga na mashoka kusafisha eneo la mradi wa
ujenzi wa kituo cha afya Kalamba kitakacho toa huduma ya mama na Mtoto,
ambapo tayari, mawe, mchanga na kokoto vimekwisha pelekwa katika eneo
la ujenzi.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Ashatu Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa
Jimbo la Kondoa Vijijini, amepongeza jitihada za wananchi hao kwa
kujitolea nguvu zao kushiriki ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho
majengo yake yatagharimu shilingi milioni 400.
Aidha, Dkt. Kijaji amesifu uamuzi wa baadhi
ya wanakijiji cha Kalamba wa kutoa maeneo yao zaidi ya ekari 6 bila
kudai fidia ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa
kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo.
Amesema
kuwa kitendo hicho kinafaa kuigwa na watanzania wengine katika maeneo
ambayo miradi ya kijamii inapita ili kuipunguzia serikali gharama za
miradi na hivyo kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Mganga
Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Dkt. Ikaji
Rashid, alisema kuwa kituo hicho cha afya kitakuwa na majengo sita
yakiwemo wodi ya wazazi, jengo la upasuaji wa dharula wa mama wajawazito, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la wagonjwa wa nje.
"Akina
mama wajawazito watakao hitajika kufanyiwa upasuaji baada ya kubainika
kuwa na changamoto ya uzazi watapatiwa huduma hapa hapa hivyo hakutakuwa
na haja ya kukimbizwa mjini Kondoa hivyo wataepuka gharama na kuepuka
kujifungulia majumbani" Alisisitiza Dkt. Rashid.
Alisema
kuwa Serikali imetoa pia fedha kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili
ya kununua vifaa vitakavyotumika kutolea tiba baada ya ujenzi wa kituo
hicho cha afya kukamilika.
Wakizungumza
katika ziara hiyo ya kukagua eneo la ujenzi wa kituo hicho kipya cha
afya Kalamba, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kondoa Bi.
Hija Bakari Suru na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilayani Kondoa
Alhaji Othman Gora wamewataka wakazi wa kata hizo mbili kujitolea
kufanyakazi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Aidha,
walisisitiza umuhimu wa kamati ya ujenzi kufanyakazi kwa bidii na kwa
uadilifu ili malengo ya muda mrefu ya wananchi wa kata hizo la kupata
huduma karibu na maeneo yao yaweze kufikiwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni