Inspekta
Jenerali wa Polisi, Simon Sirro anawashukuru Wananchi kwa ushirikiano
wanaoendelea kuutoa kwa Jeshi la Polisi jambo ambalo limesaidia
kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
Kiujumla
hali ya usalama hapa nchini ni shwari na matukio makubwa ya uhalifu wa
kutumia Silaha yamepungua kwa kiasi kikubwa na jitihada za kukabiliana
na makosa ya usalama barabarani zinaendelea ili kupunguza ajali
zinazosababisha vifo na majeruhi kwa raia.
Tunapoelekea
kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi katika mikoa yote
linawahakikishia wananchi kuwa limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sikukuu hii
inasherekewa kwa amani na utulivu na hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu
vitakavyofanyika na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi
utaimarishwa kwenye maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe,
sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko
mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi wote wanasherekea sikukuu hiyo
katika hali ya utulivu.
Wazazi
wanatakiwa kuwaangalia watoto wao na kutowaacha kutembea peke yao bila
ya kuwa na uangalizi wa karibu, pia wamiliki wa kumbi za starehe
wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi
hizo ikiwemo kutoruhusu disko toto na kujaza watu kupita kiasi.
Vilevile
Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia
barabara kuwa makini na kuzingatia Sheria za Usalama barabarani hasa kwa
madereva wa magari na pikipiki kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba
mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi
hovyo.
Nawatakia Pasaka njema.
Post a Comment
karibu kwa maoni