KAMISHNA
wa Operesheni wa Polisi (CP), Nsato Marijani amesema hadi sasa
watuhumiwa waliokamatwa kudaiwa kuhusika na kifo cha Kada wa Chadema,
Daniel John wamefikia wanne.
Pia
amesema waliokamatwa katika tukio la kuuawa kwa kukatwa mapanga Diwani
wa Kata ya Namwala Wilaya Kilombero, Geofrey Lwena wamefikia 10.
Amesema
watuhumiwa wanaodaiwa kuandamana kinyume cha sheria na kusababisha kifo
cha mwanafunzi wa Chuo cha taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwilini wamefikishwa mahakamani na uchunguzi unafanyika kwa aliyetenda.
CP Marijani ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam na kwamba upelelezi wa mauaji yote bado unaendelea.
"Kama
tulishakamata watu wanne sisi tupo kwenye nafasi nzuri ya kusema nini
kilikuwa sababu ya kifo hiki na nani waliokitenda, "amesema.
Amefafanua
kuwa hawezi kuzungumzia zaidi kwani upelelezi unaendelea na kuwataka
wananchi kuacha kusambaza taarifa ambazo hawana uhakika nazo.
Akizungumzia kifo cha Diwani Lwena, amesema wanataarifa zaidi za chanzo cha tukio hilo.
"Kadri
upelelezi unavyoendelea tutajua wahusika wakina nani na tutawafikisha
mahakamani,"amesema.Amesema vifo hivyo havihusiki na matukio ya kisiasa.
Akizungumzia maandamano, CP Marijani amesema jeshi la Polisi halitakubali kufanyika maandamano kwani ni kinyume cha sheria.
"Lolote
linalofanyika katika nchi hii sisi kama jeshi la Polisi tunawaasa
wananchi walifanye kwa mujibu wa sheria, suala la kufanya maandamano
ukiwa na nia ya kuiondoa serikali ni uhaini, "amesema.
Amewataka wazazi na walezi wawaonye vijana wao kuwa vitendo wanavyokusudia kufanya ni uhaini na ni kinyume cha sheria.
"Ni
dhahiri kwamba jeshi la Polisi haliwezi likakubali jambo hili litokee,
tutafanya kila ambalo lipo kwenye uwezo wetu, kwa kadri tunavyoruhusiwa
na sheria kuhakikisha kwamba jambo hili halifanyiki, "amesema na kuongeza;
"Sasa
tusije baadae tukalaumiana, tumelisema hili wazi tunaamini kabisa
watanzania waliokuwa wengi ni watu wazuri na wema wachache wasiotaka
kufuata sheria na wanataka kuchezea usalama wa nchi hii basi sheria
itachukua mkondo wake, "
Post a Comment
karibu kwa maoni