0
Na Theddy Challe,Babati.
WAZIRI wa viwanda, biashara na uwekazaji Charles Mwijage  amezindua eneo la ujenzi wa viwanda (Industrial sheds) lililopo katika eneo la ofisi za Sido mkoani Manyara linalotarajiwa kutoa ajira kwa watu zaidi ya 1000.
Akiwa katika ziara yake ya kushtukiza ya  kukagua maeneo ya viwanda wilaya ya Babati leo, Mwijage alisema kuwa ujenzi huo utasaidia kuanzisha viwanda vitakavyotoa  ajira, malighafi, soko na teknolojia ya uendeshaji chini ya mkandarasi Suma JKT.
Alisema Tanzania sasa tunajenga viwanda na kwamba kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli viwanda 3306 vimejengwa na vinafanya kazi.
Pia katika viwanda hivyo baadhi vimeruhusiwa kufanya kazi kwa amri ya waziri huyo na havijafunguliwa rasmi akitolea mfano wa viwanda vya vigae vya Mkuranga na  Chalinze vilivyopo mkoani Pwani, kulingana na nafasi yake na fedha iliyowekezwa viwanda hivyo vinatakiwa vifunguliwe na Rais.
“Kiwanda kipya cha kuchakata nyanya cha Dabaga mkoani Iringa kimekamilika na kinafanya kazi lakini pia kitafunguliwa na Rais mwenyewe kwa kukata utepe, wanaofikiri kwamba viwanda tunavyovianzisha vimekwishaanza na ndiyo utaratibu kazi yangu ni kuhamasisha zaidi na sio kuvifungua,” Alisema Mwijage.
Dira ya serikali ni kwamba ifikapo mwaka 2025 jamii ya watanzania iwe ni jamii ya kipato cha uchumi  wa kati lakini hatuendi kwenye kipato cha kati bali tunapita kwenye kipato cha kati kwani hicho ni kituo tu cha kufikia uchumi wa juu.
Alisema maelekeo ya chama cha mapinduzi (CCM) ilani yake inaelekeza kujenga uchumi wa viwanda na limeelekezwa katika mpango wa miaka 5 unaoweza kutufikisha katika uchumi wa kati uliojumuishi ambao utasaidia watu kuwa na hali nzuri ya kipato.
“Tukizindua gesi yetu kukafukua madini kwa fujo kipato cha Taifa kitakuwa kikubwa ukigawa kwa idadi ya watu unapata wastani wa dola elfu 3 tunachotaka sio hicho, tunataka uchumi wa kati jumuishi kwamba watu wote wawe na hali nzuri,” Alisisitiza waziri Mwijage.
Kwa mujibu wa Mwijage uchumi unaoweza kuwashughulisha wote na kuweza kupata kipato kizuri na sawa ni uchumi wa viwanda kwamba kijengwe kiwanda na kiajiri watu, kinunue malighafi za watu kwa kuwa asilimia kubwa ya watu hao ni wakulima.
“Viwanda vizuri vitakavyopendwa na watu ni viwanda ambavyo vitachakata malighafi  zinazozalishwa na wakulima, vinavyotoa ajira kwa wingi,  viawnda ambavyo bidhaa zake zinanunuliwa kwa wingi na viwanda ambavyo vinaongeza thamani ya bidhaa,”           Alieleza Mwijage.
Kwa upande wake mkurugenzi wa SIDO Taifa mhandisi Sylvester Mpanduji aliwataka  wananchi wa mkoa wa Manyara kuchangamkia fursa za uwekazaji huo na kudai kuwa hakuna sababu ya kuweka biashara katika maeneo ya makazi kwani haitatambulika kisheria.
Meneja wa SIDO mkoa wa Manyara  Mapunda alisema kuwa ujenzi wa eneo maalumu la viwanda (Industrial Sheds) lina ukubwa wa ekari 9.14 na kati ya hizo ekari 2.3 zimeendelezwa kwa kujenga ofisi ya SIDO mkoa yenye ukumbi wa mafunzo.
Alisema eneo la ekari 6.855 lilibaki ni eneo la wazi ambalo litajengwa majengo matatu ambayo yataweza kuanzishwa kwa viwanda vipya 10 ambapo viwanda vipya vilivyoanzishwa kwa kipindi cha 2015 hadi 2018 ni 350 vilivyotoa ajira kwa watu 1500 na viligharimu  sh bilioni 1.9
Naye Meneja kutoka SUMA JKT, Daudi Mabalanzengo aliwataka wauzaji wa vifaa vya  ujenzi kutokupandisha bei pindi ujenzi utakapoanza mwezi Mei kwa kuwa ajira zitalenga wakazi wa Manyara.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top