0
Leo March 13, 2018 Upande wa Mashtaka kutoka Tanzania umeiandikia nchi ya Msumbiji barua ya kuiomba msaada wa kisheria katika upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha wa USD 150,000 inayomkabili Mhasibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo, Joyce Moshi.
Hayo yameelezwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili Wankyo amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, isipokuwa wameandika barua kwenda nchini Msumbiji kuomba msaada wa kisheria (Mutual Legal Assistance) ili kufanya upelelezi wa kesi hiyo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi March 27,2018.
Mshtakiwa Mushi anakabiliwa na mashtaka 9, ikiwemo kughushi na utakatishaji fedha.
Inadaiwa October 25, 2016 katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Maputo nchini Msumbiji, alighushi barua ikionesha kwamba Ubalozi wa Tanzania nchini humo umeielekeza Benki ya Millennium kupeleka USD 10,000 katika akaunti inayomilikiwa na Joyce Moshi akijua yakuwa siyo kweli.
Pia anadaiwa katika tarehe tofauti kati ya October 25, 2016 na April 12, 2017 akiwa mtumishi  wa umma kama Mhasibu wa Ubalozi wa Tanzania aliiba USD 150,000 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia inadaiwa kati ya October 25, 2016 na April 12, 2017 katika ofisi za ubalozi huo, Moshi alijipatia dola za Marekani 150,000.
Pia inadaiwa kati ya October 25, 2016 na April 12, 2017 katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Maputo nchini Msumbiji na Benki ya Millenium BIM tawi la Julius Nyerere Maputo, alijipatia dola za Marekani 150,000 wakati akijua fedha hizo ni zao la  kughushi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top