Mke
wa mwigizaji na mchekeshaji maarufu nchini, Amri Athumani ‘Mzee
Majuto’, Aisha Yusufu (39), amewaomba Watanzania wamuombee mume wake
apone na aendelee na shughuli zake.
Mzee
Majuto ambaye alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Tumaini jijini
Dar es Salaam, Januari mwaka huu na kuruhusiwa, alirudishwa tena hapo
jana baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na kidonda kushindwa
kufunga.
Aisha amesema mume wake alifikishwa hapo akiwa katika hali mbaya lakini anashukuru kwa sasa anaendelea vizuri.
“Ninachoomba
Watanzania waendelee kumuombea tu mume wangu apone na kuruhusiwa kutoka
hospitali kwa kuwa akilala kitandani na mambo yake yanalala,” amesema.
Amesema huo ni upasuaji wa pili kwa Majuto kufanyiwa baada ya ule wa kwanza wa henia aliofanyiwa jijini Tanga Julai mwaka jana.
“Wakati
tunahangaika kuangalia namna ya kupata tiba ya nyonga ndipo
alipogundulika kuwa ana tezi dume na hivyo kufanyiwa upasuaji,” amesema.
Mzee
Majuto amewahi kucheza filamu mbalimbali ikiwemo Welcome Back, Mshamba,
Pedeshee, Si Sawa, Mama Ntilie, Nahama, Gumzo, Mrithi Wangu, Rent
House, Ndoa ya Utata, Daladala na Nimekuchoka.
Post a Comment
karibu kwa maoni