0
Majambazi wamevamia Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam na kupora fedha na baadhi ya vifaa vya kuendeshea misa usiku wa kuamkia leo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango, Uchumi na Fedha wa parokia hiyo, Arnold Kimanganu amesema kuwa majambazi hao waliwapiga walinzi kabla ya kuingia kanisani.

“Majambazi walivyofika waliwapiga walinzi, tuna walinzi wanne walimshika mlinzi mwenye silaha wakampiga na kumnyang’anya bunduki, kumkamata mwingine wakampiga na kumfunga na wakaingia sehemu inaitwa sakristia, wakavunja milango ya sakristia wakakusanya matoleo yote yaliyokuwa yamehifadhiwa yaliyokusanywa kipindi cha pasaka,” amesema Kimanganu.

Paroko wa parokia hiyo, Sunil Kishor amesema majambazi hao walivamia kanisa hilo saa tisa usiku na wameiba fedha na baadhi ya vifaa vya kuendesha misa.

“Ni kweli majambazi walivamia kanisa letu majira ya saa tisa alfajiri, walichochukua kuna pesa za sadaka ambazo zilikuwepo sakristia, vifaa vya misa hasa vikombe na siborio,” amesema Paroko Kishor na kuongeza kuwa;

“Kiasi cha fedha ambacho wamechukua kadri ya hesabu ni kama milioni nane hivi, Tumesharipoti polisi na wapo hapa kanisani wanaendelea na uchunguzi.”

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri kutokea ingawa bado hajapata taarifa ofisini kwake kimaandishi .

‘’Ni kweli vibaka walivamia na wameiba sadaka, lakini bado sijalipata vizuri tukio hili nikilipata nitalitolea taarifa, lakini nathibitisha kutokea kwa tukio hilo,” amesema Kamanda Mambosasa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top