0
Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema kazi kubwa ya usalama wa taifa ni kukusanya habari na kuishauri serikali na wala si kukamata watu kwa mabavu.

Mkuchika ameyasema hayo jana Aprili 16 bungeni wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

“Naomba nichukue nafasi hii kufafanua sheria ya usalama wa taifa inasema nini, usipojua kazi za idara ya usalama wa taifa, utawapa lawama kwa kazi ambazo si zao,” alisema.

Alisema idara hii hutekeleza majukumu kulingana na sheria ya usalama wa taifa namba 15 ya mwaka 1996 na sheria hiyo katika kifungu cha nne, inasema kazi yake ni kukusanya, kuchambua na kuishauri serikali hatua za kuchukua.

Alisema ameamua kulisema hilo kwa kuwa wabunge wengi wamezungumzia kuhusu watu wa idara ya usalama kukamata watu ovyo na kwa kutumia mabavu.

“Pili haitakuwa kazi ya idara ya usalama, kumfuatilia fuatilia mhalifu. Nimeona niiseme hiyo kwa sababu mazungumzo mengi yameelekeza huko, mtu ameuawa ni ‘polisi kesi’, hakuna nchi ambayo idara ya usalama ina shughuli ya kukamata watu,” alisema.

Alisema:  “Kama mnataka usalama wa taifa wafanye kazi ya kukamata watu basi walilete suala hilo bungeni.”

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top