Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani
amesema chama cha siasa kutangaza kugomea uchaguzi hakuwezi kuifanya
Tume iuahirishe kwa kuwa haiko kumshawishi mtu au chama kushiriki.
Akizungumza
leo Jumanne Desemba 12,2017 jijini Dar es Salaam, Kailima amesema chama
kushiriki uchaguzi ni jambo la hiari na NEC ipo kwa ajili ya kuweka na
kutengeza mazingira yatakayofanya vyama vya siasa kushiriki uchaguzi.
Kailima
katika taarifa iliyotolewa na NEC amesema iwapo kuna chama kitaamua
kutoshiriki uchaguzi, kitakachoshiriki hata kama ni kimoja mgombea wake
atapita bila kupingwa.
“Ikitokea
vyama vikasusa vyote kushiriki kwenye uchaguzi hapo ndipo unaweza
kuahirishwa kwa kuwa hakutakuwa na mgombea,” amesema alipozungumza na
waandishi wa habari waliotaka ufafanuzi wa NEC kuhusu tamko lililotolewa
na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Kailima
ameviasa vyama vya siasa vinavyotishia kutoshiriki uchaguzi mdogo wa
ubunge katika majimbo matatu na kata sita Januari 13,2018 kufuata mifumo
ya kisheria ya kushughulikia malalamiko ya uchaguzi.
Juzi
Mbowe alitishia kuwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) havitashiriki uchaguzi iwapo changamoto zilizojitokeza wakati wa
uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 Novemba 26,2017 hazitafanyiwa
kazi na NEC.
Akizungumzia hoja hiyo, Kailima amesema katika orodha ya vyama vilivyopo NEC, Ukawa si moja ya vyama vya siasa.
“Niwasihi
vyama vya siasa watumie mifumo iliyopo ya kawaida ya kuwasilisha
malalamiko kwenye kamati za maadili; kujaza fomu namba 14 kabla ya kura
kuanza kupigwa; fomu 16 wakati kura zinapigwa; na kuwasilisha malalamiko
mahakamani baada ya kura kuhesabiwa,” amesema Kailima.
Amesema
hiyo ndiyo mifumo iliyowekwa kisheria katika kushughulikia changamoto
za uchaguzi zinapojitokeza na kuhoji wanayotaka wao ni ipi.
“Kama kuna mgombea hakuridhika mahakama zipo aende maana wamepewa siku 30 za kufungua kesi,” amesema.
Amesema
NEC haiwezi kuahirisha uchaguzi kwa kuwa sheria inatamka kuwa uchaguzi
unaweza kuahirishwa iwapo tu kuna mgombea amefariki; kutokuwepo mgombea;
zikitokea ghasia na fujo au wagombea wakifungana kwa kura.
“Je kuna mgombea amefariki? Haya mambo yote manne hayajatokea, sasa tutaahirishaje uchaguzi?” amehoji Kailima.
Kuhusu
jimbo la Longido ambalo Mbowe alidai shauri la uchaguzi bado liko
mahakamani na wameiandikia NEC kuhusu suala hilo na barua kutojibiwa,
Kailima amesema madai hayo si ya kweli kwa kuwa barua zote
walizoandikiwa wamezijibu.
Amesema jimbo hilo liko wazi kwa kuwa Mahakama ndiyo imeiandikia NEC kuitaarifu kumalizika kwa kesi iliyokuwepo mahakamani.
Kailima amesema NEC itasimamisha uchaguzi wa jimbo hilo iwapo tu Mahakama itawaeleza wasimamishe mchakato huo.
“Nimesikitishwa
na kauli kwamba eti wametuandikia barua sisi Tume ya kusimamisha
uchaguzi wa Longido eti hatujawajibu. Tulipata barua kutoka kwa ole
Nangole (Onesmo) tukamjibu, tukapata barua kwa wakili wa Ole Nangole
nikamjibu; tukapata barua kutoka kwa katibu wa Chadema tukamjibu na
nikaongea naye kwenye simu, sasa leo wanaposema hatujawajibu kwa kweli
kauli hiyo imenisikitisha,” amesema
Post a Comment
karibu kwa maoni