0
Jeshi la Polisi nchini limesema operesheni zake za kila siku haziwalengi wafuasi wa chama fulani, bali linakabiliana na wananchi wenye fujo.

Lakini limesema, wakati mwingine mazingira yanapokuwa magumu ni bora jeshi hilo lipate lawama kuliko fedheha.

Akizungumza leo Aprili 4 katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Msemaji wa jeshi hilo, ACP Barnabas Mwakalukwa amesema;

“Bora kupata lawama kuliko fedheha.... maana wakati mwingine mambo yakiharibika nyie wanahabari ndiyo mnakuwa wa kwanza kuandika vichwa vikubwa vya habari ‘watu sabini wafa mbele ya askari.”

Mwakalukwa alikuwa katika kipindi hicho akifafanua kuhusu uzinduzi wa nyumba mpya za askari utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Arusha.

Amesema kuna wakati jeshi hilo linajikuta halina namna zaidi ya kutumia nguvu kubwa kukabiliana na uharibifu kuliko kuamua kutumia nguvu ya wastani na baadaye madhara yake yanakuja kuwa makubwa.

Akijibu swali la mwananchi mmoja aliyetuma ujumbe kwenye kituo hicho na kuhoji; “ kwa nini jeshi hilo limekuwa likitumia nguvu kubwa kwa wafuasi wa vyama na hata wakati mwingine kuwasukuma bila sababu”, ACP Mwakalukwa amesema:

 “ Kwanza sisi hatujui kama kuna wafuasi, tunatambua wananchi. Kama wapo hao wafuasi wanamfuata bosi wao na kumshangilia sisi tunachofanya ni kuwatawanya wananchi ili wasilete bughudha kwa wengine. Tunachofanya ni kutumia nguvu za wastani tu kulingana na nguvu tunayokabiliana nayo,” alisema.

Kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa vyama vya siasa vinavyolishutumu jeshi hilo kutumia nguvu kubwa wakati vyama hivyo vikiwa katika majukumu ya kisiasa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top