0
Spika wa Bunge, Job Ndugai ametaka kina mama wenye malalamiko ya kutelekezewa watoto na wabunge wafike kwake au wamwandikie barua kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, amesema watakapofanya hivyo wapeleke na cheti cha uthibitisho cha vipimo vya vinasaba (DNA) ili waone ni namna gani ya kushughulikia suala hilo.

Ndugai alisema hayo jana Jumanne Aprili 10, 2018 kabla ya kuahirisha kikao cha sita cha Bunge mjini Dodoma.

Katika kauli yake iliyoambatana na vicheko Spika alisema, “Kule Dar es Salaam kuna zoezi linaendelea, huko sasa kidogo kiti cha Spika kimetikiswa hivi. Tunatuhumiwa mahali, kidogo tumeguswa hivi kwa hiyo natarajia kupata ushauri wenu waheshimiwa tunafanyaje katika mazingira haya kwa maana kuna watoto wetu wako barabarani.”

“Haiwezekani hata kidogo, kwa hiyo kina mama wale inabidi tufanye utaratibu tujue nini tutafanya lakini pia kuna kina baba wamejitokeza huko nimesikia na baadhi ya walalamikiwa ni kina mama wabunge, kwa hiyo hili jambo halina upande,” alisema Ndugai.

“Hawa kina mama kama wapo, basi waje kwa spika au wamwandikie spika lakini waniletee na DNA test certificate (cheti cha uthibitisho cha vipimo vya vinasaba) ili tuone namna gani ya kuwezesha.

“Kuna mafungu hapa tumepitisha tunaweza kuangalia namna ya kuweka sawasawa ili waheshimiwa wabunge wawe na utulivu katika kufanya kazi za Bunge na si kuwa na mawazo mengine,” alisema.

Wanawake na wanaume wamekuwa wakijitokeza katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwasilisha malalamiko kuhusu kutelekezewa watoto.

Akizungumzia suala hilo jana Aprili 10, 2018 mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda alisema kati ya wanawake 480 waliosikilizwa 47 walidai wametelekezwa na wabunge.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top