Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kasoro pekee ya utaratibu ulioanzishwa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwasikiliza wanawake na
watoto ‘waliotelekezwa’ na waume zao ni kutokuwa na faragha kwa watoto.
Akizungumza
leo Jumatano Aprili 11, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha 360
kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Ummy amesema kinachofanywa na
Makonda kipo ndani ya sheria, hata watendaji wanaowasikiliza wanawake
wametoka katika idara yake.
Amesema
Wizara ya Afya inaunga mkono jitihada hizo, kwamba kasoro
zilizojitokeza ni kwa baadhi ya wanawake waliotelekezwa kwenda na watoto
na kutojali haki za kuwalinda katika hatua hizo za awali za mashtaka.
“Makonda
amefanya kitu kizuri mwamko umekuwa mkubwa, ni sawa madawati yapo na
ustawi wa jamii pia wapo lakini wengi wamekuwa wazito ila kwa sasa
wameitikia wito kwakuwa yeye amewahimiza wanawake wenye matatizo hayo
wafike kwake, kazi imekuwa nyepesi kwani hata wanaohudumia pale ni watu
wetu wa Ustawi wa Jamii,” amesema Ummy.
Amesema
kilichofanyika ni kama kuita kambi ambayo baadaye matokeo
yatakayopatikana yatawanufaisha wanawake na ikiwa kutakuwa na ugumu kesi
itakwenda mahakamani.
Hata
hivyo, Ummy ametoa wito kwa wanawake wanaokwenda kutoa mashtaka yao
kuhakikisha wanalinda haki za watoto wao kwa kutowaonyesha hadharani.
“Ninasema
hili ni kosa la mwanamke mwenyewe, kwa mfano yule mtoto Mchina
nimesikitika sana kule ni kumnyanyapaa amesambazwa mitandaoni kila
mahali anazungumziwa, niwaombe Watanzania tujitahidi kuwalinda watoto
hawa, tusisambaze picha zao kwa maslahi mazuri ya mtoto,” amesema Ummy.
Post a Comment
karibu kwa maoni