Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kufadhili mradi wa Kuongeza Mnyororo wa
Thamani wa Mazao ya Chakula ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya
Tano za kujenga uchumi wa viwanda na kuinua kipato cha wakulima.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina
Khamis Shaaban, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia
Maendeleo ya Miundombinu Vijijiji, Bw. Olagoke Oladapa, kwenye Mkutano wa Mwaka
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB unaoendelea Jijini Busan- Jamhuri ya
Korea Kusini.
Bi.
Amina Shaaban anayemwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, katika Mkutano huo,
alisema kuwa mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018, AfDB ilituma timu ya wataalam nchini
Tanzania kufanya mazungumzo ya awali na
Serikali kuhusu utekelezaji wa mradi huo ambao ni ahadi ya Rais wa
AfDB, Dkt. Akinumwi
Adesina kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Tanzania mwishoni wa mwezi
Aprili, 2018.
Miongoni
mwa viongozi wa Serikali waliokutana nao ni pamoja Mawaziri kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, na Wizara ya Mifugo
na Uvuvi.
“Serikali
imefurahishwa na utayari wa AfDB kufadhili mradi huo kwani utachangia ukuaji wa
uchumi na kuleta maendeleo katika sekta ya viwanda na kilimo nchini Tanzania”
alisema Bi. Shaaban
Naibu
Katibu Mkuu Bi. Shaaban alisema utekelezwaji wa mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani
ya mazao ya chakula utanufaisha watu wengi hasa wa kipato cha chini kwa kuwa
sekta ya kilimo Tanzania inachukua nafasi kubwa katika kuinua uchumi wa nchi.
Aidha,
Naibu Katibu Mkuu, aliahidi kuwa Serikali itaharakisha ukamilishaji wa taratibu
za maandalizi ya awali ya mradi huo utakao chochea maendeleo ya Sekta ya Kilimo
na Viwanda kwa kiasi kikubwa kwa kuwa tayari Benki ya AfDB imeonesha utayari wa
kuupatia fedha.
Imetolewa
na;
Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Post a Comment
karibu kwa maoni