0
Image result for YANGA VS RUVU 
TIMU ya Yanga SC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.
Sare hiyo inaifanya Yanga SC ijiongezee pointi moja na kufikisha 52 baada ya kucheza mechi 29 na sasa itaingia kwa mchezo wa mwisho na Azam FC ikitakiwa lazima kushinda ili kumaliza nafasi ya pili, baada ya kuvuliwa ubingwa na mahasimu wao wa jadi, Simba SC.
Iliwachukua dakika ya 18 tu Yanga kupata bao la kwanza leo kupitia mshambuliaji wake, Matheo Anthony aliyemalizia pasi nzuri ya kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
Bao hilo halikudumu sana, kwani Ruvu Shooting walifanikiwa kusawazisha dakika ya 27 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Khamis Mcha ‘Valli’, kufuatia beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja kuunawa mpira uliopigwa na Fully Maganga.
Hata hivyo, Yanga SC ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 36 kupitia kwa kiungo wake chipukizi, Maka Edward aliyemalizia pasi ya kiungo Pius Buswita aliye katika msimu wake wa kwanza Jangwani tangu asajiliwe kutoka Mbao FC ya Mwanza.
Kipindi cha pili hakikuwa kizuri kwa Yanga, kwani pamoja na kuwaruhusu Ruvu Shooting kusawazisha bao, lakini pia walijikuta wakipoteza nafasi zaidi ya tatu nzuri ya kurejesha ushindi wao. 
Aliyeisawazishia Ruvu leo alikuwa ni mshambuliaji Issa Kandru aliyefunga bao jepesi dakika ya 47 kufuatia mabeki wa Yanga kuzubaa wakidhani alikuwa ameotea naye akamalizia pasi ya Maganga kuifungia timu yake.
Yanga ilijaribu kutoka kwenda kutafuta bao lingine la ushindi, lakini pamoja na uimara wa safu ya ulinzi ya Ruvu Shooting na wachezaji wake wakapoteza nafasi tatu za wazi, ikiwemo ya Buswita mwishoni kabisa mwa mchezo.   
Pazia la Ligi Kuu litafungwa usiku wa Jumatatu ya Mei 28, kwa mechi nane, Yanga SC wakimenyana na Azam FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 2:00 usiku baada ya mechi saba za Saa 10:00 jioni, ukiwemo mchezo kato ya mabingwa, Simba SC na wenyeji, Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.
Mechi nyingine za jioni ni kati ya Lipuli na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba na Tanzania Prisons dhidi ya Singida United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ndanda FC dhidi ya Stand United Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mtibwa Sugar dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro, Njombe Mji FC dhidi ya Mwadui FC na Mbao FC dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Wakati Ligi Kuu inamalizika Jumatatu, tayari Simba SC ndiyo mabingwa wakiwa wamejikusanyia pointi 68 katika mechi 29, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 na waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 52 za mechi 29.
Njombe Mji FC tayari imeshuka Daraja kutokana na kuambulia pointi 22 katika mechi 29, wakati Ndanda FC yenye pointi 26 za mechi 29 na Maji Maji FC yenye pointi 24 za mechi 29 pia mojawapo itashuka pia baada ya mechi za Jumatatu.
Wakati timu mbili zitaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu Jumatatu, tayari African Lyon, KMC, JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara zimekwishapanda kuelekea ligi ya msimu ujao, itakayokuwa na timu 20 ambayo ni ongezeko la timu nne.
Kikosi cha Yanga; Ramadhani Kabwili, Hassani Kessi, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu, Said Juma, Maka Edward, Pius Buswita, Papy Tshishimbi/Geoffrey Mwashiuya dk82, Matheo Anthony, Thabani Kamusoko na Emmanuel Martin/Paulo Godfrey dk64.
Ruvu Shooting; Abdallah Rashidi, George Amani, Yusuph Nguya, Hamisi Kasanga, Rajab Zahir, Baraka Mtuwi, Abdulrahaman Mussa/William Patrick dk27, Shabani Msala, Issa Kanduru/Ishara Juma dk85, Fully Maganga/ Zuber Dabi dk72 na Khamis Mcha.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top