Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Mkakati wa Serikali wa kuziwezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutekeleza Miradi yenye kuchochea upatikanaji wa mapato ili ziweze kujitegemea, Jijini Dodoma. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI Mhe. Selemani Jaffo (Mb). |
Kwa mara ya kwanza katika historia
ya nchi, Serikali imezindua Mkakati wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea
upatikanaji wa mapato ili ziweze kujitegemea.
Mkakati
huo umezinduliwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu
Kijaji, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ambapo
amesema kiasi cha shilingi bilioni 131.47 kitatumika kutoa ruzuku ya
utekelezaji wa miradi 22 kwa halmashari 17 zilizoko katika mikoa 10 nchini,
katika mwaka wa fedha 2018/19.
Ameitaja mikoa hiyo ambayo
Halmashauri zake zimekidhi vigezo vya kunufaika na miradi ya kimkakati katika
awamu ya kwanza ya mpango huo kuwa ni Dar es Salaam, Geita, Kigoma,
Kilimanjaro, Lindi, Morogoro, Mtwara, Pwani, Simiyu na Songwe.
Amesema
kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Halmashuri zinajenga uwezo wa
kujitegemea kwa takribani asilimia 80 hadi 100 ifikapo mwaka 2025, badala ya
hali ya sasa ambapo halmashauri hizo zinategemea ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa
zaidi ya asilimia 88.
Amezitaka
halmashuri zitakazopata fedha za miradi hiyo kuhakikisha fedha hizo zinawekezwa
kwenye miradi yenye tija, inayokuza ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya
halmashauri.
Ametoa
wito kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kubuni miradi ya
kibiashara kwa ajili ya wananchi wanaowaongoza kwa kutengeneza ajira kwa
kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Alionya
kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watendaji wanaosimamia miradi
hiyo ikiwa watatumia fedha hizo kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa na
kurejea kauli ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwamba kufuja fedha za Serikali
katika kipindi hiki ni sawa na kunywa sumu.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, amesema
kuwa Serikali inazo fedha za kutosha kufanikisha mkakati huo na kutoa wito kwa viongozi
wa Mikoa husika kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanisha miradi yenye tija ili
ipatiwe fedha.
Alifafanua
kuwa tayari Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika mkoa wa Dar es Salaam
katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kujenga Kituo cha Mabasi cha
Mbezi Luis, Ujenzi wa Soko la Mburahati katika Manispaa ya Ubungo, Ujenzi wa
Soko la Kisasa la Magomeni katika Manispaa ya Kinondoni na Ujenzi wa Soko la
Kisasa la Kisutu, Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Vingunguti katika Manispaa
ya Ilala.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI Selemani
Jaffo (Mb) amesema kuwa Ofisi yake itaanza kufuatilia na kupima utendaji kazi
wa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ili kuona kama wanaendana na kasi ya
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliwapongeza
Wakurugenzi walioonesha mfano katika kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kubuni miradi yenye tija na ya kimkakati iliyopewa Fedha na Wizara ya
Fedha na Mipango na kuwataka watendaji wengine waige mfano huo.
Baadhi
ya miradi itakaotekelezwa na Halmashauri zilizokidhi vigezo ni pamoja na Ujenzi
wa Masoko ya Kisasa, Ujenzi wa Maegesho ya Malori, Ujenzi wa stendi za kisasa,
Maghala ya kuhifadhi mazao, Masoko ya Kisasa, Machinjio na Ujenzi wa Viwanda.
Post a Comment
karibu kwa maoni