0
Image result for YANGA SC 
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo miwili tu, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Sokoine mjini Mbeya.
Sokoine, wenyeji Tanzania Prisons watawakaribisha mabingwa watetezi, Yanga SC wakati Kirumba Ndanda FC watakuwa wageni wa Mbao FC.
Yanga kwa sasa inawania kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu, lakini pia na kuisogeza heshima ya kuitwa bingwa mtetezi angalau hadi mwishoni mwa wiki.
Kuitwa bingwa mtetezi kutakoma leo iwapo Yanga itatoa hata sare, kwani inahitaji kushinda ili kuwazuia mahasimu wao kutangaza ubingwa leo.
Simba ina pointi 65 baada ya kucheza mechi 27 na Yanga yenye pointi 48 za mechi 24, inaweza kumaliza na pointi 66 ikishinda mechi zake zote zilizosalia- maana yake hata wakitoa sare na Tanzania Prisons leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Wekundu wa Msimbazi watatawazwa kuwa wafalme wa Tanzania Bara.
Ndanda na Mbao zote zinapigana vita ya kukataa kuiacha Ligi Kuu, hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa wa upinzani na ushindani mkali.
Ndanda FC ipo nafasi ya 15 kwa pointi zake 23 za mechi 27, ikiizidi kwa pointi moja Njombe Mji FC inayoshika mkia, wakati Mbao FC ipo nafasi ya 14 kwa pointi zajke 24 za mechi 26.
Ikumbukwe timu mbili zitashuka Daraja mwishoni mwa mwezi huu na tayari JKT Tanzania, African Lyon, KMC za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Biashara United ya Mara na Alliance Schools ya Mwanza zimepanda kwa ajili ya Ligi Kuu ya timu 20 msimu ujao. 

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top