0
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, leo watakuwa kwenye uwanja wa Uhuru kuikaribisha Ndanda FC katika mechi muhimu.
Ligi hiyo leo itahusisha mechi mbili ambapo mbali na kwenye uwanja wa Uhuru, mechi nyingine itakuwa kwenye uwanja wa Majimaji Songea ambapo wenyeji Majimaji wataikaribisha Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani.
Inatabiriwa mechi ya Yanga na Ndanda itakuwa ngumu kwa kila upande, ugumu unaosababishwa na matokeo ya timu hizo tangu zilipoanza kukutana.
Kila timu itataka kutengeneza rekodi yake, Ndanda wakitaka kutunza rekodi ya kutopoteza mchezo dhidi ya Yanga wakati Yanga wakifukuzia kupunguza ‘gap’ la pointi nne dhidi ya watani wao wa jadi Simba ikiwa ni harakati za kutaka kutetea ubingwa wao.
Timu hiyo ya Jangwani ina pointi 37 mpaka sasa baada ya kucheza mechi 17 ikishinda 11 kutoka sare nne na kufungwa mbili wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Simba iliyo na pointi 41 kileleni.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina bado ana imani timu yake itafanya vizuri kwenye mechi zijazo, ikiwemo ya leo dhidi ya Ndanda na kuwataka mashabiki wa timu hiyo ya Jangwani kusahau matokeo ya sare dhidi ya African Lyon wiki iliyopita na badala yake wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu yao ili ipate matokeo mazuri.
“Ni mapema sana kupoteza matumaini ya ubingwa, mpaka sasa ligi bado ngumu huwezi kutabiri nani eti anaweza kuwa bingwa, chochote kinaweza kutokea, naamini Yanga ina nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wake,”alisema.
Simba wameipita Yanga pointi nne, ambazo ni sawa na wastani wa mechi mbili na kwamba ana matumaini ya kushinda mchezo wa leo ukiwa ni pamoja na ule wa watani zao. Hata hivyo, Yanga itabidi iombee dua mbaya Simba itoke sare au kupoteza michezo yake ili iweze kutimiza ndoto yake ya kutetea ubingwa.
Mechi zilizopita 2016-2017 Yanga inatarajia kukutana na upinzani mkali kutokana na rekodi zao za nyuma katika mchezo wa raundi ya kwanza Ndanda iliilazimisha suluhu baada kufanikiwa kucheza mchezo wa kulinda goli ‘Kupaki Basi’ hasa kipindi cha pili.
Huu ni mchezo wa sita kwa Yanga na Ndanda kukutana katika Ligi Kuu soka Tanzania bara, huku Yanga ikiwa wametoka sare mara nne na kufungana mara moja moja.
Tofauti ya nafasi katika msimamo wa 2016-17 Baada ya michezo ya mwishoni mwa juma lililopita, Ndanda inashika nafasi ya 10 baada kucheza mechi 17 imeshinda tano, imetoa sare nne na kupoteza michezo minane wakati Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza michezo 17 kushinda 11 kutoka sare minne na kupoteza miwili.
Yanga wakiwa uwanja wa Uhuru hawatakuwa na kingine zaidi ya kutafuta ushindi kwa hali na mali wakitumia vema faida ya uwanja wa nyumbani, wakati Ndanda watakuwa wakisaka pia ushindi wao wa kwanza kwenye uwanja huo dhidi ya Yanga.
Rekodi Ndanda vs Yanga Yanga imeifunga Ndanda mara moja katika mechi tano walizokutana kwenye Ligi Kuu bara. Februari 1, 2015 Yanga ikiwa mwenyeji ililazimishwa suluhu kwenye uwanja wa taifa kabla ya kuchapwa 1-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Mtwara siku ya mwisho ya kufunga msimu wa 2014/15 ilikuwa ni Mei 9, 2015.
Msimu uliopita 2015/16 mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa Januari 17, Yanga iliifunga Ndanda bao 1-0 kwenye uwanja wa taifa wakati mechi ya pili iliyotakiwa ichezwe Mtwara lakini ikahamishiwa Dar es Salaam, Ndanda waliilazimisha Yanga sare ya kufunga mabao 2-2 hiyo ilikuwa ni Mei 15, 2015.
Tangu timu hizi zimeanza kukutana, yamefungwa mabao sita (6) huku kila timu ikiwa imefunga matatu. Kila timu imepata ushindi mara moja, sare zikiwa nne na kila timu imepoteza mara moja dhidi ya mwenzie.
Telela, Chove, Makassi dhidi ya timu yao ya zamani Salum Telela itakuwa ni mechi yake ya pili dhidi ya Yanga tangu alipomaliza mkataba wake msimu uliopita na timu hiyo, mechi ya kwanza ni ile ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika kwenye uwanja wa Nangwana Sijaona, huku mlinda mlango Jackson Chove na Kiggi Makasi waliwahi kuitumikia Yanga misimu kadhaa iliyopita na leo wanakutana nayo wakiwa upande mwingine.



Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top