0
Maduka 14 katika eneo la Mianzini jijini Arusha yameteketea kwa moto jana asubuhi na kusababisha hasara mbalimbali huku jeshi la polisi likiimarisha ulinzi na kusimamia shughuli za uokoaji wa mali zilizosalimika. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye baadhi ya majokofu yaliyokuwa katika baadhi ya maduka hayo. 
Kamanda Mkumbo alisema mara baada ya hitilafu hiyo, moto huo ulishika mitungi ya gesi iliyolipuka na kuanza kusambaa kwa kasi na kuunguza maduka hayo. 
Alisema wamefanikiwa kuokoa baadhi ya mali katika maduka tisa kati ya 14 kwa msaada wa wananchi na wasamaria wema waliokuwa katika eneo la tukio lakini ukubwa wa hasara bado haujajulikana.
 Mmiliki wa moja ya maduka yaliyoteketea, Zena Athuman alisema kabla ya kufungua biashara yake, alifika katika eneo la tukio na kukuta moto huo umeshaanza na hakufanikiwa kuokoa mali yoyote kwa kuwa moto huo ulikuwa ukisambaa kwa kasi ya ajabu. 
Shuhuda wa tukio hilo, Julius Sangeti alisema alifika katika eneo hilo saa 11:30 asubuhi na kushuhudia moto ukiwaka katika duka kubwa la Mianzini na kadri muda ulivyokuwa ukisonga, ndivyo ulivyokuwa ukihamia kwenye maduka mengine na kuteketeza mali.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top