Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Fatiki Kingazi amefariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta na kusombwa na mafuriko katika kata ya Kiranyi wilayani Arumeru huku familia zaidi ya thelathini zikikosa makazi na kuhifadhiwa kwa muda kwenye vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Elkiurei.
Askari polisi waliuchukua mwili wa marehemu huku baadhi ya wasamaria wema wakiendelea na kazi ya uokoaji na kutoa maji kwenye nyumba zilizoathirika ambapo baadhi ya waathirika wamesema mvua hizo zilianza kunyesha majira ya saa nne ya usiku wa kuamikia leo.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Elkiurei Onesphori Chami amesema eneo lililokutwa na maafa lipo mkondo wa maji yanayosababisha na ujenzi holela na wamekuwa wakifikisha taarifa kwenye ngazi husika bila mafanikio.
Akizungumzia katika eneo hilo mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Ngaramtoni Sophia Shoko amewataka wale wote wanaoishi katika mkondo wa maji kuondoka ili kuepuka maafa ya mara kwa mara na kutoa siku tatu kwa watu waliyoziba mapito ya maji kufunga kabla sheria haijachukua mkondo wake.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha Charles Mkumbo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Post a Comment
karibu kwa maoni