Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi
kuendelea kusimamia na kufuatilia sheria na
miongozo yote iliyotolewa ili kuhakikisha
lengo la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima
kwenye Mashirika na Taasisi za Umma ikiwemo safari za nje na posho za wajumbe
wa Bodi za mashirika na Taasisi zote za Umma linafanikiwa.
Hayo yameelezwa Bungeni
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa (CCM), Mhe. Japhet Hasunga ambaye
alitaka kujua hatua ambazo Serikali inatarajia kuchukua kudhibiti matumizi ya fedha za Umma katika
Taasisi zake.
Dkt. Kijaji alisema
kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa matumizi ya fedha za
Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu kupitia Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge ikiwemo
Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 ambayo imebainishwa hatua mbalimbali za
kibajeti zenye lengo la kuongeza usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za
Umma katika Mashirika na Taasisi za Umma.
“Sheria hiyo
imebainisha utolewaji wa Mwongozo wa Mipango na Bajeti wa Serikali unaojumuisha
Mashirika na Taasisi zote za Serikali ambao unatoa miongozo mbalimbali
ya kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka husika”, alifafanua Dkt. Kijaji
Alisema kuwa
kupitia Sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kupitia
bajeti za Mashirika na Taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia miongozo na
mipango ya Serikali inayotarajiwa kutekelezwa.
Mhe. Kijaji
alibainisha kuwa katika Sheria hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa jukumu
la kupitia na kuridhia kanuni za fedha za Mashirika na Taasisi zote za Umma ili
kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma.
“Sheria nyingine
iliyopitishwa na Bunge ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 ambayo
iliweka ukomo kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia asilimia 60 tu ya mapato
yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha mishahara”, aliongeza Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji
alisema kuwa katika kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa Hazina inatekeleza majukumu
yake kisheria, imetoa miongozo mbalimbali yenye lengo la kudhibiti matumizi ya
Mashirika na Taasisi za Umma ili kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
“Miongoni mwa
miongozo hiyo ni barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10 Novemba, 2015
ya kudhibiti safari za nje ya nchi zisizo za lazima kwa watumishi wa Mashirika
na Taasisi za Umma ambazo awali zilionekana kutumia sehemu kubwa ya fedha za Umma”,
alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa
waraka wa Msajili wa Hazina Na. 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za Vikao vya Bodi
ya Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma pia ni miongoni mwa miongozo ya
kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwani waraka huo umefuta posho za vikao vya
Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na vikao zaidi ya vinne kwa mwaka.
Dkt. Kijaji alisema
kuwa Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2016 kuhusu posho za kujikimu
kwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma ulikuwa na
lengo la kuendeleza jitihada za Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya
fedha za Umma.
Alisema kuwa Waraka
huo uliweka ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa safari za ndani na nje
ya nchi, huku akisisitiza kuwa bado Serikali itaendelea kuhakikisha matumizi ya
fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu.
Post a Comment
karibu kwa maoni