Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto pamoja na Shirika la Afya
Duniani (WHO), inakamilisha majaribio ya utafiti wa hali ya umasikini katika
mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro kabla ya kuanza utafiti huo nchi nzima mwezi
Agosti, mwaka huu.
Hayo yamesemwa mjini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati Ujumbe kutoka Benki ya Dunia
ulipotembelea na kukagua ujenzi wa Jengo Jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa
ya Takwimu mjini humo.
Amesema kuwa ana matarajio kwamba mchakato wa taarifa
za utafiti huo zitafanywa mjini Dodoma baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi
hiyo inayojengwa kwa gharama ya shilingi 11.6 bilioni, zikiwa ni fedha za mkopo
wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Dkt. Chuwa ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano
kwa wakusanya taarifa za utafiti huo ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi za
hali ya umasikini nchini kwa ajili ya kutathmini programu mbalimbali na kupanga
mipango ya maendeleo ya wananchi wake.
Nae Mshauri wa Masuala ya Kitakwimu kutoka Benki ya
Dunia nchini Tanzania, Elizabeth Talbert amesema kuwa Benki yake imetoa mkopo
huo kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara na Zanzibar
kutokana na Benki hiyo kuona mchango mkubwa wa takwimu katika maendeleo ya nchi
yoyote ile duniani.
“Tumefurahishwa na kasi ya ujenzi wa Ofisi hii hapa
mjini Dodoma na tunaamini ujenzi wake utakamilika kwa wakati ili kazi za
kitakwimu ziweze kufanyika katika
mazingira mazuri na tunaamini hatua hii italeta mchango mkubwa katika masuala
ya kitakwimu hapa nchini” alisema Bibi Talbert.
Amesema kuwa Jengo la Ofisi ya Takwimu kwa upande wa
Zanzibar limekamilika na huenda likaanza kutumika mapema Julai mwaka huu hatua
ambayo inaleta mageuzi makubwa katika tasnia hiyo ya ukusanyaji wa takwimu
mbalimbali zinazoisaidia nchi kupanga mipango ya maendeleo ya watu wake.
Post a Comment
karibu kwa maoni