SERIKALI
imepokea gawio la zaidi ya shilingi bilioni 10 kutoka taasisi tatu ikiwemo TPB
bank, na kampuni mbili za mafuta za Tiper na Puma ambazo serikali inamiliki
hisa zake.
Taasisi
ya kwanza kuwasilisha gawio hilo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango mjini Dodoma ni Benki ya TPB ambayo mwenyekiti wake Profesa Lettice
Rutashobya amekabidhi hundi kifani ya shilingi bilioni 1.032, ikifuatiwa na
Kampuni ya kuhihadhi mafuta ya Tiper iliyowasilisha gawio la shilingi bilioni
2.
Kampuni
ya mafuta ya Puma ikahitimisha zoezi hilo kwa kukabidhi hundi kifani ya
shilingi bilioni 7 ambazo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 14 ambazo
kampuni hiyo imepata baada ya kulipa kodi.
Akizungumza
katika tukio hilo lililofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Mjini
Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amezipongeza taasisi hizo
na amezitaka Taasisi za Serikali na mashirika ya umma kuilipa Serikali gawio la
hisa zake na zijiendeshe kwa ufanisi na kwa faida ili makusanyo hayo yaweze
kuwahudumia wananchi.
Dkt.
Mpango amerejea kauli yake aliyoitoa bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha
Bajeti Kuu kwamba Serikali itatoa kipaumbele kwa kufanya biashara na taasisi
zake za Umma ili ziweze kujiimarisha kimapato na hatimaye kutoa gawio
Serikalini.
“Leo
ni siku nzuri sana kwa watanzania kwa sababu Serikali inapokea gawio la
shilingi bilioni 10 kwa niaba yao lakini fedha hizi hazitoshi nataka mfanye
vizuri zaidi ili gawio liweze kuongezeka ili tuzielekeze kutatua kero
zinazoikabili jamii ikiwemo elimu, afya na maji” alilisisitiza Dkt. Mpango.
Katika
tukio hilo pia, Benki ya TPB Plc imelipatia Shirika la Posta kiasi cha shilingi
milioni 97.8 ikiwa ni gawio kulingana na hisa zake asilimia 7.98 inazomiliki
katika Benki hiyo.
Akipokea
hundi kifani ya kiasi hicho cha gawio, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Shirika la Posta nchini, Dkt. Haruni Ramadhan Kondo, ameiomba Serikali ililipe
shirika lake kiasi cha shilingi bilioni 3.6 ambazo ni malipo ya pensheni ya
wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Jumuiya ya Afrika Mashariki
ambapo Shirika limelipa pensheni hizo kwa niaba ya Serikali ili liweze kuongeza
mtaji na kujiendesha kwa faida zaidi.
Awali
Wenyeviti wa Bodi za wakurugenzi wa Taasisi hizo wameahidi kuendelea kufanya
biashara kwa umahili mkubwa ili kuongeza gawio kwa wanahisa wake na kuiomba
iwawekee mazingira yatakayosaidia kufanikisha azma yao hiyo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPB Bank, Profesa Lettice Rutashobya, amesema kuwa
Benki yake imeendelea kukua kwa kasi, kuimarika na kufanya vizuri katika
biashara ya fedha pamoja na kuwa mahili katika ubunifu na kuwa tishio kwa
taasisi nyingine za fedha.
Nae
Meneja wa Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta-Tiper, Bw. Emmanuel Kondi, ameiomba
Serikali kuiwezesha kampuni hiyo kufanya biashara kwa mafanikio zaidi hivyo
kuongeza gawio ikiwemo kuangalia upya mfumo wa himaya moja ya Forodha ambao
amesema pamoja na kuwa na ufanisi mkubwa una baadhi ya changamoto.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Kuuza Mafuta-Puma,
Dkt. Ben Moshi amesema kuwa Kampuni yake ilitengeneza faida na kuiwezesha kutoa
gawio la shilingi bilioni 7 kwa Serikali ikilinganishwa na shilingi bilioni 4.5
ilizotoa mwaka wa fedha uliopita.
Utaratibu
wa Taasisi za Serikali na mashirika ya umma kulipa gawio la hisa kwa Serikali
na wanahisa wengine ni maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuhakikisha kuwa Taasisi hizo zinafanya
kazi kwa ufanisi, kuzalisha faida na kutoa gawio kwa Serikali ili mapato hayo
yaweze kuhudumia wananchi katika Nyanja mbali mbali kama vile huduma za afya,
elimu, maji na barabara.
Post a Comment
karibu kwa maoni