WAKAZI wa
Jiji la Arusha wameondokana na na adha ya umeme kukatika mara kwa mara
baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme katika Kituo cha kupoozea umeme
cha Njiro kilichoko Mkoani Arusha chenye uwezo wa kuzalisha megawati 130.
Hali hiyo
inatokana na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kuwekeza kiasi cha Dola milioni
4.2, ukiwa ni mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili kuongeza uwezo wa Kituo
hicho kuzalisha umeme unaotumika kwa ajili ya makazi ya watu, maeneo ya
biashara na viwanda.
Msimamizi Mkuu
wa Kituo cha Usambazaji umeme cha Njiro Mhandisi Lembrice Mollel amesema mradi
huo umesaidia kuongeza Megawati 130 za umeme ambao umekidhi
mahitaji ya Jiji la Arusha linalo hitaji Megawati 60 hivyo kubakiwa na Umeme wa
ziada kiasi cha Megawati 70.
Alisema kuwa
tatizo la kukatika katika kwa umeme katika mji huo wa kitalii na kibiashara
litakuwa historia na kwamba umeme unaozalishwa kituoni hapo unasafirishwa
kwenye maeneo mengine yenye uhitaji ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Kwa upande wake
Meneja wa Mradi wa Umeme wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi
Frorence Gwang’ombe amesema kuwa lengo la mradi lilikuwa kupatikana kwa umeme
wa uhakika na kuimarisha miundombinu ya usambazaji na kupooza umeme jambo
ambalo limefikiwa kikamilifu.
Alisema kuwa
uboreshaji wa Kituo hicho cha kupoozea Umeme cha Njiro ni sehemu ya utekelezaji
wa uboreshaji wa Sekta ya Umeme nchini kupitia mradi ujulikana kama Electricity
V, uliofadhiliwa na AfDB kupitia mkopo nafuu wa kiasi cha Dola milioni
8, ukihusisha pia mkoa wa Dar es Salaam, Vituo vya kupooza umeme vya Sokoine na
Ilala.
“Mradio huu
umelenga kuwahudumia wananchi takribani 8,400 hivyo kukamilika kwa mradi huo ni
neema kwa wananchi wengi kwa kuwa utasaidia kuimarisha uwezo wao wa kibiashara
ndani ya Jiji la Arusha na maeneo mengine ya nchi” alisema Mhandisi Gwang’ombe
Alifafanua kuwa
uboreshaji wa mradi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Njiro umehusisha ufungaji wa
transfoma mpya 2 zenye uwezo wa kufua megawati 50 kila moja na nyingine 2 zenye
uwezo wa kubeba megawati 15 kila moja, hatua iliyosaidia kuongeza kiwango hicho
cha umeme.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), anayehudumia Kanda ya Afrika
Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, ameelezea kuridhishwa na utekelezaji pamoja
na manufaa ya mradi huo utakaosaidia kukuza biashara na kusisimua uwekezaji wa
viwanda katika mkoa wa Arusha.
‘Arusha ni mji
wa Kitalii hivyo unahitaji kuwa na umeme wa kutosha utakaosaidia katika
uwekezaji na ufanisi wa biashara, upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea shughuli
za Kilimo na viwanda kwa kasi kubwa’, aliongeza Dkt. Weggoro.
Amewataka
wakazi Arusha na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za kiuchumi
zinazotokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya umeme ili kwenda sambamba na Sera
ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Baadhi ya
wakazi wa Mji wa Arusha, wakiwemo Bw. Jackson William na Bw. Steven Chitara
wamekiri kuwa maisha yao yamebadilika kiuchumi kutokana na kuimarika kwa
upatikanaji wa umeme ikilinganishwa na hapo awali.
Wamesema kuwa
vijana wengi wamejiajiri kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali
zinazotegemea uwepo wa nishati hiyo kama kuchomelea vyuma, vinyozi, ufundi wa
aina mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wakubwa kuanza kuvutiwa kuwekeza
mkoani humo.
Post a Comment
karibu kwa maoni