0
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amezindua Kitabu cha Mwongozo kwa Wanamipango Tanzania, kilichoandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Jamii ya nchini Uholanzi (ISS), na kuwataka wataalamu wa mipango hapa nchini kuandaa mipango yenye tija itakayoiwezesha jamii kuondokana na umasikini.

Dkt. Kijaji ameeleza kuwa nafasi ya wataalamu wa mipango katika kukuza uchumi wa nchi ni kubwa na kwamba kinachotakiwa ni kuandaa mipango shirikishi itakayochangia kuimarisha maisha ya wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Ni matumaini yangu makubwa kwamba kuzinduliwa kwa kitabu hiki cha mwongozo kwa wanamipango, kutakuwa chachu ya wataalamu wetu kuangalia namna ya kupeleka maendeleo vijijini na sehemu nyingine duniani kwa kutoa wataalamu waliobobea ili kuharakisha maendeleo ya nchi” alisistiza Dkt. Kijaji

Ameeleza kuwa maudhui ya kitabu hicho yapelekwe hadi ngazi za chini kupitia Serikali za Mitaa ili watu wengi waweze kukisoma na kuelekezwa namna bora ya kupanga mipango yao ya maendeleo.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijini, Prof. Hozen Mayaya, amesema kitabu hicho kimelenga kuwaongezea ujuzi wataalamu wa mipango kwa kuzingatia vitendo zaidi badala ya nadharia.

“Kitabu cha Mwongozo kwa wanamipango kitakuwa rejea ya nadharia nyingi na njia ambazo wataalamu wanapaswa kuzijua, namna ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuifanya mipango iweze kutekelezeka kama ilivyokusudiwa” alisema Prof. Mayaya.

Nae Kaimu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Bi. Lianne Houben, ambaye kwa namna moja au nyingine nchi yake imefadhili uandishi na uchapaji wa mwongozo huo, toleo la pili, amesema nchi yake inajivunia uhusiano imara uliodumu kwa miongo kadhaa na Tanzania.

Alisema kuwa mtazamo wa ushirikiano wake na Tanzania kuanzia mwaka huu ni kujikita zaidi katika uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na kwamba uwekezaji wao mkubwa utalenga pia kuboresha kilimo na usalama wa chakula.

“Uholanzi ni nchi ya pili katika kufanya biashara na Tanzania ikitanguliwa na Marekani ambapo mwaka 2016, Uholanzi, imenunua bidhaa zenye thamani ya Euro bilioni 85” aliongeza Bi. Houben

Aidha, alieleza kuwa nchi yake imetoa mchango mkubwa katika kuendeleza rasilimali watu ambapo hadi sasa wanafunzi na wataalaamu katika fani mbalimbali wapatao 5,000, wamepata mafunzo kutoka katika vyuo mbalimbali nchini Uholanzi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top