0
WATUMISHI wa umma, madereva na wanafunzi wa sekondari na vyuo vya elimu ya juu, sasa watalazimika kupimwa mkojo, damu na nywele ili kubaini kama wanatumia dawa za kulevya au la.
Hatua hiyo ambayo bila shaka itadhibiti kwa kiwango kikubwa matumizi ya dawa za kulevya nchini, itafanywa wakati wa usaili wa wafanyakazi ili kuajiriwa, usaili wa madereva kabla ya kupewa leseni au wakati wa udahili wa wanafunzi wanapojiunga na shule au vyuo husika.
Hata hivyo mpango huo utahusisha taasisi za umma au shule zitakazoomba kwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili wafanyakazi wake au wanafunzi wapimwe vipimo hivyo wakati wa usaili na udahili. Kwa upande wa madereva, mpango huo utatekelezwa endapo Jeshi la Polisi au vyombo vinavyowasimamia usafiri vitaomba hivyo. Hayo yamebainika Dar es Salaam jana na Meneja Sayansi Jinai wa Maaabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima alipozungumzia kuanza kutekelezwa kwa mpango huo.
“Lengo la mpango huu kwanza ni kusaidia kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya maana vijana wengi ambao ndio wanafunzi na wanaoajiriwa sasa wataogopa kwa kujua kuwa jamii au ndugu watawabaini, lakini pia itasaidia kusaidia tiba kwa waathirika,” alisema Mulima. Meneja huyo alisema kutokana na maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa na vifaa vya kisasa, majibu ya vipimo hivyo yatachukua muda wa kati ya siku 2 hadi 30 kulingana na utumiaji wa aina ya dawa za kulevya.
Aliongeza kuwa kwa cocaine na heroine, majibu hupatikana kuanzia siku mbili huku bangi majibu yatatoka kati ya siku 28 hadi 30. Alisema vipimo vya mkojo, damu au nywele, ndivyo vinavyotumiwa na maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, huku kipimo cha mkojo kikitumiwa zaidi kutokana na kutoa majibu kwa haraka, kikifuatiwa na kipimo cha damu na baadaye nywele, lakini vyote vikitoa majibu kwa muda usiopungua siku mbili au kuzidi siku 30. “Pamoja na kuanzisha mpango huu, lakini si kwamba tutakwenda katika kila taasisi na kupima.
Tutawapima wafanyakazi wa umma, wanafunzi au madereva wale tu ambao taasisi zao zitaomba kwetu tufanye hivyo pengine baada ya kubaini mwenendo usio sahihi kwa watu wao. “Mtumishi wa umma anaweza kuwa anasinzia mara kwa mara ofisini, au ajali nyingi unaweza kuona kuwa kutokana na dawa za kulevya aina ya heroin kusababisha usingizi basi dereva alisinzia na ajali ikatokea.
Ni vema watu hawa sasa wakaripotiwa kwetu ili tuwapime,” alisema Mulima. Alisema utekelezaji wa mpango huo, utawezesha kuongezeka kwa ufanisi katika utumishi wa umma, shuleni na vyuoni, lakini pia utapunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya kuwa eneo kubwa linaloathiri ufanisi katika maeneo hayo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top