0
Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amekutana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Barclays Kanda ya Afrika, Bw. Peter Matlare na kuiomba Benki hiyo kuangalia uwezekano wa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa viwango vya kimataifa (SGR) mradi wa miundombinu ya umeme wa Stieglar's Gorge ili kurahakisha maendeleo ya kiuchumi kupitia viwanda.

Amemweleza kiongozi huyo kwamba Serikali imeimarisha uchumi Mkuu kwa kudhibiti mfumuko wa bei ambao uko katika kiwango chatarakimu moja cha wastani wa asilimi 5.3 katika kipindi cha miezi 6 iliyopita.

"Tumewekeza kwenye miundombinu kama vile Elimu, maji, kilimo, afya, madini, na biashara na kwamba katika kipindi kifupi cha miaka 2 zaidi ya viwanda 80 vimejengwa katika eneo la Mkuranga mkoani Pwani, kutokana na fursa za uwepo wa bomba la gesi na eneo hilo kuwa karibu na Bandari ya Dar es Salaam.

Dkt. Mpango ameelezea pia mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) ambao amesema utarahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo katika nchi zinazopakana na Tanzania hivyo kukuza biashara kwa kiwango kikubwa.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika Bonde la mto Rufiji (Stiegler's Gorge), Dkt. Mpango amesema lengo la mradi huo utakao zalisha megawati 2,100 za umeme utakao kuwa wa uhakika na bei nafuu ili kukuza viwanda.

Alisema kuwa mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa kila biadhaa zinazozalishwa nchini pamoja na madini, vinaongezwa thamani hapa hapa nchini badala ya kuuzwa kama malighafi na kwamba nishati ya umeme ndiyo nguzo kuu ya kufikia malengo hayo.

"Ili tuweze kufikia azma hiyo tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika na wa bei nafuu ili viwanda vyetu viweze kuzalisha kwa wingi ndio maana tunaiomba Benki yako iweze kufikiria namna ya kushiriki katika ujenzi wa miradi hii" Alisisitiza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango ameipongeza Benki ya Barclays ambayo pia ni mwanahisa katika Benki ya NBC kwa ahadi yake ya kutaka kuwekeza kiteknolojia katika sekta ya benki nchini hatua ambayo itasaidia kukuza mitaji na mikopo kwa kundi kubwa la watanzania wakiwemo wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa.

Alielezea msimamo wake kwamba katika kukuza uchumi, Serikali inathamini mchango mkubwa wa Sekta Binafsi na imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba hivi karibuni alikuta na wadau wa Sekta ya Benki ili kusikiliza changamoto zao na pia kuwaeleza mambo muhimu ambayo ingependa sekta Binafsi ifanye ili kufikia malengo yanayokusudiwa.

Awali, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo ya Barclays anaye hudumia kundi la benki za Barclays Barani Afrika na kwingineko Marekani na Ulaya, Bw. Peter Matlare, ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kusimamia kikamilifu uchumi wa nchi unaokua kwa wastani wa asilimia 7.

Alisema hatua hiyo ni ya kupigiwa mfano katika nchi za Kiafrika na Duniani kwa ujumla ambapo amesema Tanzania imekuwa ikifanya vyema katika kukuza uchumi jumuishi unaowafikia watu wengi zaidi wakiwemo waishio mijini na vijijini.

Bw. Peter Matlare amemhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kwamba Benki yake itayafanyia kazi mapendekezo ya kutaka ushiriki wake katika ujenzi wa miradi mikubwa iliyoainishwa na Serikali kuwa kipaumbele chake.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top