0
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameipa siku
tano Chadema kuwasilisha maelezo ya tuhuma za uvunjifu wa Sheria na
maadiliya Vyama vya Siasa  kwa kufanya maandamano Februari 16.


Barua hiyo ya Februari 21 yenye kumbukumbu namba HA. 322/362/16/34
kwenda kwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, inakitaka chama
hicho kikuu cha upinzani nchini kuwasilisha maelezo yake kabla ya
Februari 25.


“Kuwasilisha maelezo kuhusu tuhuma za uvunjifu wa sheria ya vyama vya siasa na maadili ya vyama vya siasa,”
kinasema kichwa cha habari cha barua hiyo ikirejea maandamano ya chama
hicho yaliyofanyika Februari 16 kutoka Mwananyamala kwenda ofisi ya
msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni kumtaka awapatie viapo vya
mawakala wake wa uchaguzi uliofanyika Februari 17.


Msajili wa vyama vya siasa nchini awaibukia chadema

Katika maandamano hayo, kuliibua vurugu baina ya polisi na
waandamanaji eneo la Mkwajuni na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa
mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwilini (22) baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala.


Barua hiyo ya Msajili inasema;


“Katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za ubunge za
chama chenu za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni, uliofanyika
viwanja vya Mwananyamala kwa Kopa Dar es Salaam. Inaeleza kuwa
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliongea lugha za kuchochea vurugu
ambazo zinakatazwa na Kifungu cha 9(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa
Sura ya 258 (RE: 2002) na Kanuni ya 5(1) ya Maadili ya Vyama vya Siasa
(GN. 215/2007).



“Natambua tuhuma hizi pia ni za jinai na zinafanyiwa kazi na
taasisi nyingine za Serikali. Hata hivyo, sanjali na hatua hizo, Sheria
ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, vinanitaka
nami kuchukua hatua kwa vile Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndiyo
inayosimamia utekelezaji wa sheria hizo mbili,” inaeleza barua hiyo na
kuongeza,



“Hivyo, kwa barua hii, nakitaka chama chenu kuwasilisha
maelezo ya kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, kwa kukiuka Sheria
ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, kwa
kuchochea wananchi kuandamana bila kufuata utaratibu wa sheria na
kufanya vurugu.”



Msimamo wa Chadema


Jana, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema,
John Mrema alisema walipokea barua hiyo juzi na huenda wakaijibu leo
huku akimtaka Msajili kutoingilia mamlaka zingine ambazo zimekwisha
kuanza kulishughulikia suala hilo.


“Hoja ya Msajili anasema tumeitisha maandamano kinyume cha sheria na
anasema kwa nini asituchukulie hatua. Wakati anaandika barua hiyo anajua
kabisa maandamano ni haki yetu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa
na kwa mujibu wa Katiba.


“Kama maandamano yalifanyika ni suala la polisi si Msajili na
kama ni jinai si kazi ya Msajili na kama anasimamia sheria mbona
tulipozuiwa kufanya maandamano na mikutano ambayo ni haki yetu
hakuingilia kati na kueleza sheria na Katiba inavunjwa ila hili kaliona…
Ni haki yetu kuandamana asifikiri sheria imefutwa au imebadilika bado
ni ileile mpaka sasa.”



Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Jaji Mutungi hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo na kusema, “Waulize kama wameiona barua inasema nini na mimi na wao tutawasiliana sio wewe.”

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top