0
Baada ya jana pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2017/18 kufungwa, limeacha timu mbili za Majimaji na Njombe Mji zikiaga ligi kuu na kwenda ligi daraja la kwanza huku timu nyingine sita zikipanda ligi kuu.
Mashabiki wengi wamekuwa wakijiuliza kwanini zishuke timu mbili na zipande sita, East Africa Television imemtafuta Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura na ameweka wazi sababu hizo.
Wambura amesema Bodi pamoja na TFF, wameamua kuongeza idadi ya timu kutoka 16 zilizoshiriki msimu huu hadi 20 msimu ujao, hivyo katika mapendekezo wakakubalina zishuke timu mbili kisha zipande sita ili kukamilisha timu 20.
''Ni mabadiliko ya kanuni na muundo wa ligi, tumeamua kuanzia msimu ujao tuwe na timu 20, ili kuongeza ushindani na mechi kwa wachezaji wetu ili wawe na muda mwingi wa kucheza kitu ambacho kitawajenga na hatimaye kufanya vizuri kwenye timu ya taifa'', amesema.
Aidha Wambura amesema kuanzia msimu ujao, kanuni zinaeleza jumla ya timu tatu zitashuka daraja na timu tatu zitapanda ligi kuu. Timu zilizopanda msimu ujao ni Biashara Mara, Alliance Schools, KMC, JKT Tanzania, Coastal Union na African Lyon.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top