0
SERIKALI imeitaka Sekta ndogo ya Benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo ya muda
mfupi na mrefu ambayo itawezesha ukuaji wa sekta za viwanda na kilimo pamoja na
wajasiriamali wadogo.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof.
Florens Luoga, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, katika
Mkutano wa wadau wa Sekta ya Fedha uliowashirikisha wabunge, washirika wa Maendeleo,
wakuu wa Taasisi za fedha na Wizara ya Fedha na Mipango.
Prof. Luoga alitoa wito huo kufuatia kuwepo kwa changamoto katika Sekta hiyo ikiwemo
ukosefu wa uwekezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika viwanda, kilimo na
miundombinu pia ukosefu wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Kuna kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima za kilimo, gharama kubwa za
huduma za fedha, mifumo hafifu ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha, ukosefu wa
elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi wengi kutofikiwa na huduma za fedha ambapo ni
asilimia 8.6 tu ya nguvu kazi ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki
ikilinganishwa na asilimia 32.1 ya nguvu kazi kwa wanaoishi mijini” alisisitiza Prof Luoga
Gavana huyo wa Benki Kuu alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali
ilifanya maboresho ya Sekta ya Fedha katika eneo la ubinafsishaji wa benki za Serikali
kurekebisha na kutunga sera na sheria mbalimbali hadi kufikia Desemba, 2017 ili kuweka
misingi imara ya kuwezesha ukuaji, ushindani na ufanisi katika sekta ya fedha.
“Maboresho ya Sekta ya Fedha yamesaidia ongezeko la idadi ya benki na taasisi za fedha
kufikia 54, kampuni za bima 31, kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa 27, taasisi
za huduma ndogo za fedha takriban 450, mifuko na program za Serikali 34, vikundi vya
kifedha vya kijamii takribani 30,019 katika mikoa 18 ya Tanzania bara na uanzishwaji wa
soko la bidhaa” alieleza Prof. Luoga.
Alisisitiza kuwa taasisi za fedha zikitimiza wajibu wake, sekta binafsi itakuwa na uwezo wa
kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa viwanda, kuongeza uzalishaji wa bidhaa
zitakazouzwa nje ya nchi na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa na kupunguza umasikini wa
kipato wa wananchi.
Aidha Serikali katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi, inaandaa Mpango Mkakati wa
Maendeleo ya Sekta ya Fedha, unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za

fedha, kulinda watumiaji wa huduma za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, uthabiti
wa sekta ya fedha, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha,
kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya sheria, kanuni na
taratibu katika sekta hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu, akizungumza
kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James, alisema kuwa azma ya Serikali
ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha uchumi wa nchi unaongozwa na viwanda ifikapo mwaka
2025.
“Kuwepo kwa viwanda vingi italeta ongezeko la ajira kwa wananchi walio wengi pamoja na
kuiongezea Serikali mapato” alieleza Dkt. Kazungu
Aidha, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo, ni
lazima wapate rasilimali fedha kutoka kwenye taasisi kama vile benki na masoko ya mitaji
hivyo watoa huduma kwenye taasisi hizo wanapaswa kuongeza ubunifu kwenye utoaji wa
huduma zinazokidhi mahitaji ya wapokeaji huduma kulingana na shughuli wanazofanya na
kwa gharama nafuu.
Alizitaka taasisi za fedha kuwekeza katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa
kutumia taasisi hizo kwa kujiwekea akiba na kupata mitaji itakayowezesha kukuza biashara
na shughuli zao za kiuchumi hivyo wadau wa sekta ya fedha wanapaswa kujiuliza ni kwa nini
mikopo ya biashara kwenda kwenye sekta binafsi hairidhishi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin
Kamuzora aliwataka wadau wa sekta ya fedha kuzungumzia mafanikio ya Sekta ya fedha
kwa njia ya miamala ya Simu za mkononi kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa Duniani
katika eneo hilo na hivyo kuwa mfano kwa mataifa mbalimbali.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel
ameitaka Sekta binafsi inayonufaika na mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kuwekeza
kwenye miradi yenye tija na kulipa mikopo yao kwa wakati pamoja na kuongeza thamani ya
bidhaa wanazozalisha na kuongeza kiwango cha mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi,

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top