0

Watu watano kati ya 16 wakiwemo wasanii wa kikundi cha Matarumbeta  cha mjini Babati mkoani Manyara wamefariki dunia baada ya gari  walilokuwa wakisafiria kutoka mjini Babati kwenda kwenye sherehe za kumuaga bibi harusi kwa wazazi wake( maarufu kama send off) kuacha barabara kuu kutoka mjini Babati kwenda mkoani Arusha katika eneo la Changarawe - Makatanini na kisha kupinduka.



Ajali hiyo iliyotokea majira ya saa moja kasoro usiku, imelihusisha gari aina ya Nissan pick Up yenye namba za usajili T 444 BSH  ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kama baba Maria inadaiwa iliwapeleka wacheza show na wasanii  mjini Babati kupiga picha kabla ya kwenda kumuaga bibi harusi,na ndipo ilipopinduka huku baadhi ya majeruhi wakidai huenda chanzo kimesababishwa na dereva kumkwepa mbwa.



Nae mganga mfawidhi wa haospitali ya halmashauri ya mji wa Babati ya Mrara Bw Gabriel Sonu amethibitisha kupokea miili ya watu wanne waliofariki papo hapo wakiwemo wasichana wawili  na mdogo wa bibi harusi wakiwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Joshua sambamba na majeruhi 11.


Hata hivyo kamanda wa polisi mkoani Manyara Bw Francis Jacob amethibitisha tukio hilo kupitia  taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, na kuwataja waliokufa kuwa ni Ramadhani Juma na mpuliza tarumbeta aliyejulikana kwa jina moja la Anthony mkazi wa Arusha,wengine ni Gradnes Charles na Martha Jackson ambao ni wanafunzi,huku taarifa hiyo ikieleza chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kushindwa kulimudu gari hilo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top