Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amewaonya mawakala wa forodha katika
mpaka wa Tanzania na Zambia wa Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya
kuwachelewesha madereva wa malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi ili
wapewe rushwa.
Prof. Mkenda ametoa onyo hilo katika
mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi
ya madereva wa malori waliodai wamekuwa wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa
zaidi ya siku tatu hadi tano.
Wadereva hao wameeleza kuwa mawakala
wa forodha wamekuwa wakiwaambia kuwa nyaraka zao zinazohusika na mizigo
wanayosafirisha zimekuwa zilicheleshwa na kituo cha Forodha upande wa
Zambia.
Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya
Mapato Zambia (ZRA), Kituo cha Nakonde, Bw. Nase Lungu, amekana kuhusika na
ucheleweshaji huo na baada ya ukaguzi wa moja ya nyaraka hizo ilibainika kuwa
upande wa Zambia unatoa nyaraka hizo kwa wakati lakini zimekuwa zikifichwa na
Mawakala wa Forodha upande wa Tanzania.
Wakitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo,
madereva hao wamesema kuwa mawakala wa forodha kwa muda mrefu wamekuwa
wakiwaeleza kuwa mtandao wa intaneti wa Upande wa Zambia unaotumika kuchakata
nyaraka zao uko chini, hivyo walitakiwa kutoa shilingi 10,000 kwa kila nyaraka
ili "kurahisisha" kazi hiyo kwa kuwapa kitu kidogo maafisa wa forodha
wa Zambia.
"Mawakala wengine wa forodha
wana nyumba zao za kulala wageni hapa Tunduma kumbe wanatulazimisha kukaa hapa
ili tulale kwenye nyumba hizo hali inayotutia hasara na wanatumia kutokujua
kwetu kutudanganya kwamba mtandao uko chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia
huko Zambia" alieleza kwa masikitiko dereva mmoja
Baada ya kubaini uwepo wa vitendo
hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf
Mkenda, ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA upande wa Tunduma kuandika
kibao chenye namba za simu za Mkuu wa TRA mpakani hapo zitakazotumiwa na
madereva wanaocheleweshwa kwa makusudi kutoa malalamiko yao.
"Tunataka madereva mtumie siku
moja tu kukamilisha nyaraka zenu ili muendelee na safari yenu vinginevyo
tutadumaza biashara kati ya Zambia na Tanzania na pia tutaifanya Bandari yetu
ya Dar es salaam kushindwa kuleta tija" aliongeza Prof. Mkenda
Alisema kuwa wakala wa forodha
atakayebainika kufanya mchezo huo mchafu wa kuwarubuni madereva na
kuwachelewesha kupeleka mizigo nchini Zambia, watanyang'anywa leseni zao za
biashara.
Meneja Msaidizi wa Forodha wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania, mikoa ya Songwe na Mbeya, Bw. Jomimassa Nsindo,
amesema kuwa ofisi yake itashirikiana na madereva kukomesha vitendo hivyo
ambavyo amesema vinaharibu uchumi na biashara mpakani hapo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Momba, mkoani
Songwe, Bw. Juma Irando, alisema kuwa ataitisha kikao cha Madereva, Mawakala wa
Forodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde
mapema, ili kuweka msimamo wa serikali na kuwaeleza wahusika wanaokiuka
taratibu hatua watakazochukuliwa.
Prof. Mkenda na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, walikwenda katika mpaka
huo wa Tunduma na Nakonde, kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha
Pamoja cha Mpakani kati ya Tanzania na Zambia, unaotarajiwa kuanza Februari
mosi, 2017, baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya nchi hizo mbili, juzi.
Post a Comment
karibu kwa maoni