0

 
CHAMA cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania kimebaini kuwa kuna watoto wenye ugonjwa wa kisukari 1,326 katika vituo 14 kati ya 33 vya ugonjwa huo vilivyopo nchini.

Akizungumza na BLOG YAKO jana, Meneja wa Mradi wa Watoto katika Mpango wa Taifa wa Kisukari, Herieth Mganga alisema kwa sasa wameanza kuandikisha upya watoto wenye tatizo hilo, ambao inakadiriwa kuwa idadi ya watoto wenye ugonjwa huo ni 2,000 nchi nzima.

Mganga alitaja vituo ambavyo wamekwishapokea idadi ya watoto kuwa ni Singida, Dodoma, Bugando, Mbeya, Bombo, KCMC Kilimanjaro, Mount Meru, Sekou Toure, Kagera, Karagwe, Pemba, Zanzibar, Temeke na Muhimbili.

“Tuna kliniki 33 kwa ajili ya kisukari, lakini mpaka sasa tumepata majina ya watoto katika vituo hivyo 14, tunaendelea kuwasajili katika vituo vilivyobaki,” alieleza Mganga.

Katika orodha hiyo ya vituo, alivitaja vituo ambavyo vina watoto wengi wagonjwa wa kisukari kuwa ni Singida, KCMC, Meru, Bugando, Muhimbili, Zanzibar, Temeke na Bombo.

“Hivyo ni vituo ambavyo idadi ya watoto ni zaidi ya 150 katika kila kituo, lakini hiyo inatokana na pengine huduma zao ni nzuri zaidi au hakuna kituo kingine maeneo ya karibu, haimaanishi kwamba ugonjwa wa kisukari uko juu zaidi katika maeneo hayo,” alieleza Mganga.

Alisema watakamilisha kuorodhesha watoto wenye tatizo hilo Aprili 13, mwaka huu na kupata idadi kamili ya wagonjwa itawasaidia kuboresha huduma na ufuatiliaji mzuri. Alisema mpaka sasa wamekwisha toa elimu kwa wahudumu wa afya 2000 na pia wanaendelea kutoa dawa kwa wagonjwa na pia kuwagharamia vipimo vya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Mpango wa Taifa wa Kisukari, John Gardner, zaidi ya watu milioni 1.9 wana kisukari na kwamba katika kila watu 100, watu tisa wana ugonjwa huo.

“Hatuna idadi kamili, lakini ukweli ni kwamba idadi kamili ni zaidi ya hiyo, na ni kutokana na kwamba watu wengi wanaishi na kisukari lakini hawajajua kama wanaugonjwa huo,” alieleza meneja huyo alisema Gardner.

Alisema nchi nzima kuna vituo hai 148 ambavyo vinatoa huduma ya tiba na vipimo, na kwamba idadi ya ugonjwa huo inaongezeka kila mwaka na hiyo ni kutokana na aina ya maisha ambayo wanaishi watu kwa sasa.

“Unakuta watu wanakula chakula bila kula matunda na mboga kwa wingi, hawafanyi mazoezi, jambo ambalo linafanya kuwa na magonjwa mbalimbali pamoja na kisukari,” alieleza Gardner.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top