Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora imetangaza kutoa vibali vya ajira 10,184 ili kuziba nafasi
zilizoachwa wazi na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu,
imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais, Utumishi, Florence Temba, ilieleza
kuwa agizo hilo linazihusu Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa,
Wakala wa Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ilimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki akitoa agizo hilo wakati
akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa Umma wa Wilaya ya Kigamboni
mkoani Dar es Salaam jana.
Kairuki aliongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgawo
wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi
nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri
watumishi wapya kuziba nafasi wazi zilizojitokeza.
Alieleza kuwa serikali imetoa kibali kuajiri
watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye
orodha ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti
baada ya zoezi la uhakiki.
Aprili mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti
yenye orodha ya watumishi wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti
pungufu, vyenye utata na vya kughushi kutokea kwa Waziri Kairuki.
Waliokuwa na vyeti vya kughushi walikuwa 9,932, na
Rais aliapa kwamba hawatarudi kazini. Rais Magufuli aliagiza kufutwa kazi kwa
wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo na kuzuia mishahara yao ya mwezi huo, lakini
hata hivyo bado mlango uliwekwa wazi kwa wenye pingamizi na wapo waliokataa
rufaa huku wengine wakienda kwenye mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa suala
hilo.
Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro
alitangaza kuwa wiki hii serikali itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya
afya vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili
ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato kwenye
vituo vya afya na zahanati.
Post a Comment
karibu kwa maoni