Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum
Mhe. Josephine Chagulla (CCM), aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwapa wanawake
elimu kuhusu mikopo pamoja na kufikisha huduma za kibenki maeneo ya vijijini
ili waweze kufikiwa na huduma za kifedha.
Mhe.
Josephine Chagulla ameeleza kuwa wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa
sababu benki haziwafikii, pia hawana mafunzo maalumu ya kuwasaidia ujuzi wa
namna ya kuzifikia huduma hiyo ya kukopeshwa
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, elimu ya fedha inahusisha wadau mbalimbali
ikiwemo Serikali na Taasisi zake, ambapo kwa upande wa Serikali, Benki Kuu
inaratibu uanzishwaji wa taasisi ya kitaifa itakayokuwa na jukumu la kuratibu,
kuwezesha na kusimamia utoaji wa elimu ya fedha kwa jamii.
“Serikali
kupitia Benki Kuu imetoa mwongozo wa Uwakala wa Huduma za Kibenki ili kupanua wigo
wa huduma za kibenki kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa gharama nafuu
hasa katika maeneo ya vijijini”. Alisema Dkt. Kijaji.
Alisema
kuwa baada ya kuunda taasisi ya kitaifa ya Uratibu wa Elimu ya Fedha,
kutakuwepo na mfumo rasmi nchini wa utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa
wananchi wote wakiwemo akina mama wa vijijini.” Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt.
Kijaji alifafanua kuwa, Taasisi za fedha zina utaratibu wa kutoa elimu ya fedha
kwa wateja wao wakiwemo wanawake ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanaendesha biashara zao kwa ufanisi.
“Serikali
inatambua umuhimu wa wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao,
pia inatambua umuhimu wa taasisi hizo katika kuwasaidia wananchi kujikwamua
kiuchumi.” Alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha,
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua benki nyingi zinaendesha shughuli
zake mijini kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa miundombinu muhimu kwa ajili
ya uendeshaji wa shughuli za kibenki.
Katika
swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Josephine Chagulla (CCM), alitaka
kujua mpango Serikali wa kufungua matawi ya benki ya Wanawake katika mikoa yote
ya Tanzania ili kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa urahisi.
Swali
hilo lilijibiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu, ambaye aliahidi kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango
ili itimize ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ya
kuipatia mtaji Benki ya Wanawake Tanzania ili iweze kufungua matawi nchi nzima
na kutoa mikopo yenye masharti nafuu ikilinganishwa na benki nyingine.
Post a Comment
karibu kwa maoni