
Utafiti wa kinga ya kuzuia maambukizi ya virusi vya
Ukimwi, ulioanza kufanywa nchini miaka kadhaa iliyopita umeana kuonyesha
mafanikio.
Lakini watafiti wamesema Watanzania watahitaji kuwa
uvumilivu wa miaka michache ijayo kusubiri hatua za mwisho za ukamilishaji
utafiti wa kinga hiyo kabla haijaanza kutimika rasmi.
Taarifa hizo zinakuja ikiwa wiki moja baada ya Kenya
kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutumia dawa ya ugonjwa wa Ukimwi
ambayo inaweza kuboresha afya na kurefusha maisha ya maelfu ya watu ambao
wanasumbuliwa na magonjwa nyemelezi na ambayo hayakubali tiba nyingine.
Kwa miaka kadhaa Chuo Kikuu cha Afya na Tiba
Muhimbili (MUHAS) imekuwa ikiendesha utafiti kuhusiana na chanjo ya maambukizi
ya virusi vya Ukimwi na katika hatua ya awali utafiti huo uliwahusisha baadhi
ya watu wanaishi na virusi hivyo.
Akizungumzia hatua zilizofikiwa tangu kuanzishwa kwa
utafiti huo, mkurugenzi wa mafunzo endelevu na weledi wa MUHAS, Dk Doreen Mloka
amesema ingawa bado ni mapema kubainisha utafiti huo lakini kwa ujumla wake
umeanza kuzaa matunda.
Amesema matokeo ya awali yanaonyesha kuwa watu
waliopatiwa chanjo hiyo wamekuwa na maendeleo mema kwa afya zao kuimarika
maradufu tofauti na wale wanaotumia dawa nyingine za kawaida.
Amesema kutokana na matokeo hayo wataalamu
wanaofanyia uchunguzi chanjo hiyo sasa wanatengeneza mkakati maalumu ambao
unaweza kuchukua muda wa miaka mitano hadi sita kabla ya chanjo hiyo kuanza
kutumika rasmi.
“Tumepiga hatua kubwa katika utafiti huu kwa vile
tumeona kuwa wagonjwa waliopewa kinga hii afya zao zimeimarika na kiwango cha
kinga mwili kinapanda lakini siyo kwa kiwango tulichotarajia lakini kuna
utofauti na walivyokuwa wakitumia chanjo za awali,” amesema.
Mtaalamu huyo ameeleza kuwa baadhi ya dawa zinazotumika
sasa zimebainika kuwa na hali ya usugu kutibu magonjwa nyemelezi hivyo watafiti
wanaendelea kukuna vichwa vyao kusaka majibu yatakayosaidia kupendekezwa kwa
dawa mbadala.
Wiki iliyopita Serikali ya Kenya ilitangaza kuanza
kutumia dawa mpya inayotambulika kwa jina la Dolutegravir (DGT) ambayo inatajwa
kuwa ni chaguo la kwanza kwa watu wanaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) katika
nchi za watu wenye kipato kikubwa kwa kuwa zina athari chache kuliko dawa za
ARV zinazotumiwa sasa( yaani kidonge kimoja kidogo kila siku).
Mwaka 2015 Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)
lilipendekeza DGT iwe chaguo la kwanza watu wazima na vijana, lakini hadi
katika siku za hivi karibuni watu wanaoishi na VVU katika nchi kama Kenya
walikuwa hawezi kupata dawa hizo.
Kuhusu kutumika kwa dawa kama hiyo nchini, Dk Mloka
alisema inaweza kutumika lakini bado wataalamu wanaendelea na utafiti kubaini
kiwango cha usugu kwa dawa zinazotumika sasa kutibu magonjwa nyemelezi.
“Tunaendelea na utafiti ili kujiridhisha kwamba sisi
tupo sawa na Kenya tuingize dawa mpya ama tuendelee na zile za zamani kwa
sababu kuleta dawa mpya ni gharama sana,” amesema.
Ukimwi bado upo na unaua chukua thadhari,tumia
kinga.
Post a Comment
karibu kwa maoni