0
Responsive image
Kamati ya watu tisa iliyoundwa na Serikali mkoani Mbeya kuchunguza ajali ya moto katika Soko la Sido Mjini Mbeya, imemaliza kazi yake, na kubaini kuwa chanzo cha moto huo ilikuwa ni jiko la mkaa ambalo liliachwa ndani ya kibanda mojawapo sokoni hapo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hassan Mkwawa ametoa ripoti hiyo mbele ya mkutano wa hadhara uliokuwa chini ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala na kueleza hasara iliyopatikana kutokana na moto huo kuwaa zaidi ya Shilingi Bilioni 14.2.
Pamoja na hasara hiyo iliyopatikana, wafanyabiashara walichokuwa wakikisubiri ni kibali cha wao kuendelea na shughuli zao hapo sokoni, baada yakuingia wasiwasi wa kutokuruhusiwa kuendelea na biashara zao hapo SIDO.
Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makala ameamuru wafanyabiashara hao takribani 3,136 waendelee kufanya biashara zao kama kawaida na kujenga vibanda vya kudumu kwa usimamizi wa wataalam wa Jiji la Mbeya.
Makala ametoa maamuzi hayo ya kuwaruhusu wafanyabiashara hao, zikiwepo tetesi za mmiliki wa eneo hilo la Soko kupeleka shauri Mahakamani kuzuia eneo hilo lisitumike na wafanyabiashara hao .
Soko la SIDO limeteketea Agost 15 mwaka huu na kusababisha zaidi ya vibanda 2,000 kuteketea kwa moto vikiwa na mali mbalimbali za biashara, ambapo serikali ililazimika kuunda Kamati ili kupata ukweli na mapendekezo ya kufanyika ili tukio la moto lisijirudie.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top