0
Mfanyabiashara Yusuf Manji akirudishwa mahabusu baada ya kesi yake ya maombi ya dhamana kuahirishwa hadi Agosti 25 mwaka huu.
MASHAHIDI wawili wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara maarufu nchini, Yussuf Manji kuwa uchunguzi wa sampuli ya mkojo uliopimwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ulikutwa na chembechembe za dawa ya kulevya.
Naibu Mkuu wa Upelelezi Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ramadhan Kingai (42) alidai kuwa Februari 9, mwaka huu alimpokea Manji aliyefika kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi na kuamuru mtuhumiwa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupimwa kama anatumia dawa za kulevya au la.
Kingai ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi Cyprian Mkeha. Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Timon Vitalis, Kingai alidai amri hiyo aliitoa kutokana na tuhuma zilizoripotiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwamba mshitakiwa anatumia na kujihusisha na dawa za kulevya.
Alidai kuwa akiwa Mwenyekiti wa Kamati kuhusu dawa za kulevya, alielekeza mshitakiwa apelekwe kwa mkemia ambapo alimpa jukumu hilo Koplo Sospeter. Alieleza agizo lake lilitekelezwa, na baadaye alipata taarifa ya uchunguzi kwamba mtuhumiwa huyo anatumia dawa za kulevya na alitaka afunguliwe jalada la kesi.
Aliiambia mahakama hiyo kuwa jalada hilo lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na kufunguliwa mashitaka na mshitakiwa kufikishwa mahakamani. Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Koplo Sospeter (49) alidai kuwa Februari 9, mwaka huu alitumwa na Kingai kumpeleka Manji kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutoa sampuli ya mkojo.
Sospeter ambaye ni Ofisa katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alidai kuwa aliwasilisha fomu namba 001 ya maombi ya uchunguzi na kupata namba ya maabara.
Alidai baada ya kupata usajili, alimpeleka Manji msalani akiwa na chupa ya plastiki kwa ajili ya kuweka sampuli hiyo ya mkojo ili ifanyiwe uchunguzi. Hata hivyo, shahidi huyo aliomba mahakama kupokea fomu hiyo kama kielelezo cha ushahidi kwa kuwa anaitambua fomu hiyo kwani ina jina lake na saini yake. Hakimu Mkeha alikubali kupokea fomu namba 001 kama kielezo mahakamani hapo na kuahirisha kesi hiyo hadi leo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top