Baadhi ya wafugaji wamesema kuwa Soko hilo linalojengwa kwa
gharama ya shilingi milioni 650, limewaondolea adha kubwa waliyokuwa wakiipata
walipokuwa wakiuza mifugo yao nchini Kenya kutokana na gharama kubwa ya
kusafirisha mifugo kwenda huko pamoja na kulipa kodi na ushuru
mbalimbali.
Wamesema kuwa kujengwa kwa somo hilo ni mkombozi mkubwa kwao na
kwamba hali hiyo itasisimua uchumi wao kwa kuwa wafanyabiashara wa ndani na
kutoka Kenya wamekuwa wakiwafuata kwenye soko hilo kununua mifugo yao hatua
inayowafanya wapate faida kubwa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Bw. Toba Nguvila, amesema
kuwa soko hilo ambalo ujenzi wa miundombinu yake umekamilika kwa asilimia 85
limeanza kuiingiza Serikali mapato yake ambapo kwa wastani Halmashauri ya
wilaya inakusanya wastani wa shilingi milioni 1 kwa siku.
“Asilimia 95 ya wakazi wa wilaya yetu ni wafugaji wa kimaasai
ambao kwa kipindi kirefu wameteseka kusafirisha mifugo yao kwenda Kenya na
kutopata faida kutokana na gharama kubwa ya kusafirisha, kupitisha mifugo
kwenye maeneo ya watu hivyo kulazimika kulipa ushuru, halikadhalika kulipia
tozo mbalimbali wakati wakisubiri kuuza mifugo yao” alieleza Bw. Nguvila
Alisema kuwa kuanzishwa kwa soko hilo litakalokuwa na
miundombinu muhimu kama vile mizani ya kupimia uzito wa mifugo yao kabla ya
kuiuza, si tu kwamba limesababisha wafugaji kupata faida kwa kuuza mifugo yao
kwa bei nzuri ya soko, bali pia limeleta neema kwa wafanyabiashara wengine
wadogo wakiwemo mamalishe.
“Akina mama wanafanyabiashara zao za kuuza chai na chakula huku
kundi kubwa la vijana waliokuwa wakiuza bidhaa zao za kutembeza mikononi katika
mpaka wa Kenya na Tanzania-Namanga, ambao wamejiajiri kwa shughuli za kushusha
na kupakia mifugo kwenye malori” aliongeza Bw. Nguvila
Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa mifugo inaongezewa thamani,
mchakato wa kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama
kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata mifugo 3,000 kwa siku kinatarajiwa kujengwa
katika eneo la karibu na soko hilo kwa ajili ya kuuza nyama ndani na nje ya
nchi
“Taratibu za kuanzishwa kwa kiwanda hicho zimekamilika na wakati
wowote ujenzi wake utaanza hatua ambayo tunaamini watu wetu watanufaika zaidi
na biashara ya mifugo kuliko ilivyokuwa hapo awali ikiwa ni juhudi za Serikali
ya aAwamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi wa hali ya chini ili kuboresha maisha
yao” alisisitiza katibu Tawala huyo
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika anayesimamia nchi 7 za Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje
Weggoro, amesema Benki yake imefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko hilo
litakalochochea uchumi wa wananchi.
Ameahidi kuwa Benki yake inafadhili ujenzi wa masoko mengi ya
namna hiyo hapa nchini na nchini nyingine za Kiafrika ili nchi hizo ziweze
kukuza uchumi wake na maisha ya watu wake kwa ujumla.
“Benki iko tayari kuendelea kusaidia eneo hili la ujenzi wa
masoko ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi hivyo naushukuru uongozi wa
mkoa wa Arusha na Wilaya ya Longido kwa kazi nzuri wanayoifanya kusimamia
ujenzi wa soko hili na kwamba ujenzi wake utakamilika kwa wakati kama
ilivyopangwa”Alisisitiza Dkt. Weggoro.
Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB inafadhili ujenzi wa masoko
kadhaa Tanzania Bara na Visiwani kupitia mkopo wenye masharti nafuu wenye
thamani ya Dola za kimarekani milioni 56 na unatekelezwa kupitia mpango wa
kuendeleza miundombinu ya masoko, kuongeza thamani ya mazao na uboreshaji wa
huduma za kifedha vjijini.
Post a Comment
karibu kwa maoni