
Askari polisi Mjini Babati akiwa
Lindo Bank ya NMB tawi la Babati majira ya jioni amemuua kwa kumpiga risasi nne
mwanamke mmoja ambaye inasemekana ni mzazi mwenzake baada ya kumfuata na kudai
matumizi ya Mtoto.
Jeshi la Polisi wilayani Babati
Limesema linamshikilia askari huyo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU),Cosmas James akituhumiwa kumuua mzazi mwenzake, Regina Daniel (23) kwa
kumpiga risasi nne katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Chanzo cha mauaji hayo inadaiwa ni mzozo
ulitokea Regina alipomfuata James lindoni kudai fedha za matumizi ya mtoto.
Akithibitisha tukio hilo, Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Longinus Tibishubwamu amesema lilitokea
mjini Babati Ijumaa Oktoba 27,2017 saa 12:30 jioni.
Amesema askari huyo alikuwa lindoni
katika Benki ya NMB tawi la Babati, mtaa wa Usalama, Kata ya Bagara.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu amesema
Regina ni mkazi wa Mtaa wa Ngarenaro mjini Babati.
Amesema uchunguzi wa awali
unaonyesha kabla ya kifo cha mwanamke huyo kulitokea mzozo kati ya wawili hao
kuhusu fedha za matumizi ya mtoto.
"Wakati wakiendelea na mzozo,
ndipo askari huyo kwa kutumia silaha aliyokuwa nayo alimpiga Regina risasi nne
kwenye paji la uso, kifuani na shingoni," amesema.
Amesema askari huyo alitumia silaha
aliyokuwa nayo lindoni aina ya SMG mali ya Jeshi la Polisi.
Baada ya tukio, amesema askari huyo
aliitelekeza silaha lindoni na kwenda kujisalimisha polisi. Amesema askari
waliokwenda eneo la tukio waliokota maganda matatu ya risasi na waliichukua
silaha hiyo.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu amesema
mtuhumiwa yupo mahabusu kwa mahojiano kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa na
mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mji wa Babati Mrara.
Askari wa FFU mjini Babati,
aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema anashangazwa na tukio hilo
kutokana na upole alionao James.
Amesema James ni askari mwenye
nidhamu, hivyo hafahamu jambo gani limempata hadi kuchukua uamuzi wa kumuua mzazi mwenzake.
Post a Comment
karibu kwa maoni