Anaandika Benny
Mwaipaja kutoka Dar es Salaam
SHIRIKA
la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limesema liko tayari kushirikiana na
Serikali kujenga miundombinu ya kisasa ya usafiri, Nishati ya umeme, maji na
usafi wa mazingira katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Ahadi
hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Bw. Hiroshi Kato wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, Jijini Dar es Salaam.
Bw.
Kato alisema kuwa mradi mwingine wanaotaka kuutekeleza katika mji wa Dodoma ni
udhibiti wa taka ngumu na kwamba wanachosubiri ni Serikali kuainisha maeneo ya
vipaumbele vilivyoko katika mpango mji wa Dodoma.
Aidha
Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa Shirika lake litaendelea kusaidia eneo
la kilimo hususan kilimo cha mpunga ili kuongeza thamani ya zao hilo na
kuwakomboa wakulima.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amelishukuru Shirika hilo kwa kuonesha
nia ya kusaidia ujenzi wa mji wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya nchi.
Alisema
kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuupanga mji wa Dodoma mapema ili
kuondoa changamoto za msongamano wa huduma za jamii kwenye eneo moja kama
ilivyo Jijini Dar es Salaam.
“Pamoja
na umuhimu wa miundombinu ya maji, umeme, usafiri wa mjini, lakini pia tunataka
tujenge mapema njia za juu (ring roads) ili kudhibiti msongamano wa magari”
alisema Dkt. Mpango.
Aliongeza
kuwa mradi mwingine wa kipaumbele katika mji huo ni ujenzi wa uwanja wa ndege
wa kimataifa katika eneo la Msalato, karibu kilometa 20 kutoka katikati ya mji
huo ili kurahisisha usafiri kwa njia ya anga.
Post a Comment
karibu kwa maoni