Hali ya mapato ya Halmashauri ya Mji
wa Babati mkoani Manyara imeelezwa kuwa sio nzuri kulinganisha na matumizi
ambapo matumizi ya kawaida ya kulipa umeme, maji, usafi na matumizi mengine
yanakaribia shilingi milioni 200 kwa mwezi huku mapato ni wastani wa shilingi
milioni 140.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa
Babati, Mohamedy Kibiki alibainisha hayo katika kikao cha Baraza la
Madiwani kilichokuwa kikitathimini hali
ya ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo ili
viende sambamba na utoaji huduma kwa wananchi.
Alisema kasi ya ukusanyaji wa mapato
ni lazima iboreshwe ili ilingane na matumizi kwani huwezi kukusanya kidogo na
kuwa na matumizi makubwa halmashauri hiyo itakwama na itashindwa kujiendesha na
kuendesha vikao mbalimbali.
“Hali sio nzuri tunatakiwa tutoke
hapo,tuhakikishe tunasimamia na kuboresha mapato ya Halmashauri yetu,mapato hayo
yataendelea kushuka ikiwa hatutakuwa
wabunifu na kuacha kufanyakazi kwa mazoea” Alisema Kibiki.
“Ni muhimu tuwe wabunifu, tuboreshe
vyanzo vya mapato na kubuni vyanzo vipya ili kupunguza mzigo wa ukusanyaji
fedha na hatimaye kuweza kutoa huduma stahiki kwa wananchi”. Alisema.
Wananchi wanaweza kuhoji Halmashauri
yoyote kwa kushindwa kuwatolea huduma stahiki pamoja na kufanya vikao vya
kikatiba vinavyohusu maendeleo ya eneo lao.
Alibainisha kuwa madiwani wakishirikiana
na watalaamu wataweza kusimamia kikamilifu suala la uvamizi wa maeneo ya shule
kwa kupima eneo hilo, uvamizi wa viwanja vilivyopimwa katika eneo la Makatanini
na kuepusha migogoro inayoweza kuepukika.
Pia kufuatilia ujenzi holela wa
vichochoro mbalimbali vilivyovamiwa na wananchi na kujenga stoo za kuhifadhia vifaa, uzoaji wa
taka ngumu katika vizimba na kuondoa karakana bubu katikati ya mji huo ili
kuboresha afya za wakazi wa mji huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Babati,Fortunatus Fwema aliliambia Baraza hilo kuwa
Halmashauri hiyo haina vyanzo vingi vya mapato jambo ambalo husababisha
kushindwa kuendeleza miradi ya maendeleo na kubaki kusubiri ruzuku kutoka Serikali kuu ambazo huja kwa
maelekezo maalum.
Post a Comment
karibu kwa maoni