Anaandika Julieth Peter Mererani.
Serikali
imetenga shilingi milioni 700 milioni kwa ajili ya kuanzisha mradi wa
maji kwenye Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara
utakaopunguza kero ya maji kwenye eneo hilo.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji Isack Kamwelwe ameyasema hayo jana kwenye ziara
yake ya siku moja Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Waziri Kamwelwe alisema Mradi huo wa maji utasababisha asilimia 85 ya wananchi wa mji huo kupata maji ya uhakika.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwani fedha za mradi huo zimeshatengwa tayari.
Alimuagiza
meneja wa mamlaka ya maji safi Babati (BAWASA) mhandisi Idd Msuya
kuhakikisha mradi huo wa Mirerani unaanza ndani ya muda wa miezi sita.
"Baada
ya Rais John Magufuli kufanya ziara yake hivi karibuni kwenye mji mdogo
wa Mirerani alitoa ahadi ya kupatiwa maji wananchi wa eneo hilo hivyo
nikiwa Waziri mwenye dhamana hiyo amehakikisha agizo hilo
limetekelezwa," alisema Waziri Kamwelwe.
Alisema
baada ya Rais Magufuli kuagiza maji ya uhakika yapatikane Mirerani na
zoezi la ujenzi wa ukuta wa kuzunguka machimbo ya Tanzanite kuanza, yeye
kama Waziri aliamua ashughulikie suala la maji Mirerani.
Kwa
upande wake, meneja wa Bawasa, mhandisi Idd Msuya alitoa ahadi kwa
Waziri kuwa watasimamia ipasavyo mradi huo wa maji na kuhakikisha
unaanza ndani ya muda wa miezi sita.
Mkuu wa
wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa
kuitembelea kwa mara ya pili Simanjiro na kuahidi neema ya maji kwenye
miji ya Mirerani, Orkesumet na kijiji cha Naisinyai.
Chaula
alisema wilaya hiyo ina vipaumbele vitatu vya elimu, afya na maji,
hivyo ziara hiyi imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani kipaumbele chao
kimojawapo cha maji kitapatiwa ufumbuzi.
"Umekuwa
Waziri mchapakazi tangu ukiwa Naibu wa Wizara hii na kila tukikupigia
simu juu ya mradi wa maji wa kutoka mto Ruvu hadi Orkesumet ulikuwa
unatupa ushirikiano wa kutosha," alisema mhandisi Chaula.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Jackson Sipitieck alimshukuru Rais
Magufuli kumpandisha cheo Waziri Kamwelwe kuwa Waziri kamili wa Wizara
hiyo, ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo.
Sipitieck
alisema Waziri Kamwelwe ni mchapakazi mahiri kwani hii ni mara yake ya
pili kufika wilayani Simanjiro kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji.
Alimshukuru
Waziri Kamwelwe kwa kufuatilia ipasavyo mradi mkubwa wa maji kutoka mto
Ruvu hadi Orkesumet kwani utasaidia wananchi na mifugo kupata maji ya
uhakika.
"Pia tunashukuru kwa kukubali ombi
letu la kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa eneo la bwawa la Langai
linalotegemewa na wafugaji wa kata tatu za Langai, Loiborsoit na
Naberera ambalo lilipasuka na kusababisha maji kupungua ghafla na
kukauka," alisema Sipitieck.
Post a Comment
karibu kwa maoni