0
Moyo wa mwanadamu
UPASUAJI wa kuzibua mishipa ya moyo bila kufungua kifua kwa kupitia mshipa wa damu wa mkono kwa wagonjwa 33 uliofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) umeibua maajabu mapya kwa taasisi hiyo inayozidi kujipatia umaarufu mkubwa duniani.
Kwa mara ya kwanza tangu taasisi hiyo imeanza kutoa huduma ya matibabu ya upasuaji wa moyo bila ya kufungua kifua, hatimaye imeweza kufanya upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono.
Awali wakati huduma hiyo iliponzishwa katika taasisi hiyo ya JKCI, upasuaji uliokuwa unafanywa kwa wagonjwa waliofika hospitalini hapo ulikuwa ni ule wa kutumia mishipa ya paja.
Hata hivyo katika tukio la hivi karibuni, madaktari bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia walifanya upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa wagonjwa hao 33.
Upasuaji huo wa moyo uliofanyika katika kambi hiyo ya JKCI ambayo ilianza Novemba 15, mwaka huu hadi jana ni ya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa watu wazima. Pamoja na kuwepo kwa faida mbalimbali kutokana na upasuaji huo, utafiti wa gazeti hili umebaini kutokea kwa maajabu mbalimbali kutokana na upasuaji huo.
Ajabu la kwanza la upasuaji huo ni ule ambao sasa utamwezesha mgonjwa kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea tofauti na upasuaji wa awali ambapo mgonjwa hakuweza kutoka kwenye chumba cha upasuaji akiwa anatembea.
Hiyo ilitokana na upasuaji wa awali kufanyika kwa kutumia mishipa ya paja ambapo mgonjwa alikuwa analazimika kupasuliwa paja ili kupata mishipa yake iliyokuwa inatumika katika kufanya matibabu hayo ya moyo.
Ajabu la pili kutokana na upasuaji huo mpya na wa aina yake; ni lile la mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya moyo bila kufungua kifua kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya saa nne tangu afanyiwe upasuaji.
Hatua hiyo ni tofauti na upasuaji wa awali wa kutumia mshipa wa paja ambapo mgonjwa alikuwa analazimika kukaa hospitali kwa zaidi ya saa 24 ili kuangalia maendeleo ya afya yake.
Ajabu la tatu katika matibabu hayo ni hatua ya wageni hao kutoka Taasisi ya IIRO kujifunza vitu vingi na kupata uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa na mambo ya kiteknolojia katika Taasisi ya JKCI ambayo katika nchi yao hakuna.
Mufti awafumbua macho
Watanzania Akizungumzia matibabu hayo ya aina yake jana; Shehe Mkuu wa Tanzania; Mufti Abubakar Zubeir aliwaasa Watanzania kupata matibabu hasa ya magonjwa ya moyo hapa nchini ili kuepuka gharama za kwenda kupata matibabu nje ya nchi ambako gharama yake ni kubwa.
Shehe Zubeir alitoa mwito huo katika hafla ya kuwaaga madaktari hao bingwa wa IIRO wa Saudi Arabia waliofika nchini kushirikiana na wenzao wa JKCI katika upasuaji huo. “Kazi iliyofanywa hapa ni kuhakikisha watu wanapata tiba nzuri, watu wasiende nje ya nchi kutibiwa kwani gharama yake kwa mtu mmoja ni zaidi ya shilingi milioni 30, niwashitue Watanzania kuwa tiba hizi zinapatikana hapa kwenye taasisi hii ya JKCI,” alisema.
Alisema gharama ambayo mgonjwa atakwenda kutibiwa nje ya nchi ni kubwa ambapo si watu wengi wanaweza kuimudu ndiyo maana serikali pamoja na taasisi nyingine wameomba kambi hizo za matibabu kuja nchini kufanya matibabu na pia kutoa ujuzi wa madaktari waliopo.
Mkurugenzi JKCI ahimiza upimaji wa afya
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema kambi hiyo ya madaktari kutoka Saudi Arabia ilienda sambamba na kutoa mafunzo kwa madaktari wa JKCI na pia kubadilishana ujuzi kitu ambacho kimewajengea uwezo.
“Faida ya upasuaji wa aina hii ni kumuwezesha mgonjwa kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea mwenyewe na baada ya saa nane anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali kama anaendelea vizuri, kwa hiyo kambi hii ni faida sana kwetu,” alisema Profesa Janabi.
Aidha aliwasisitiza wananchi kupima afya zao mara kwa mara jambo ambalo litawasaidia kujua kama wana matatizo ya moyo hivyo kupata tiba kwa wakati. “Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni kuwa wagonjwa wengi tunaowapokea ni mioyo yao kuwa katika hali mbaya.”
Aliishukuru taasisi ya IIRO kwa kutuma wataalamu hao kuja kutoa huduma ya matibabu ambayo iliambatana na mafunzo kwa madaktari wa taasisi ya JKCI.
Balozi, Wizara wasifu ushirikiano
Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mohammed bin Mansour Almalik alisema kuja kwa madaktari hao ni ishara kwamba Tanzania na Saudi Arabia wana ushirikiano mzuri, alisema ushirikiano huo hautaishia kwenye sekta ya afya pekee bali pia katika sekta nyingine.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima alisema wizara hiyo itaendeleza ushirikiano wa aina hiyo na taasisi mbalimbali ili wataalamu wa ndani katika sekta ya afya wapate ujuzi wa kutosha na pia kujifunza teknolojia mpya kuepuka gharama za kumpeleka mgonjwa kutibiwa nje ya nchi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top