Anaandika Benny Mwaipaja.
WAZIRI wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, amezindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za
utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, utakaogharimu
shilingi bilioni 10 zilizotolewa na Benki ya Dunia.
Lengo la utafiti huo utakaofanywa
na Ofisi Kuu ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kupata takwimu zinazohusu shughuli za
kijamii na kiuchumi, mapato na matumizi, hali ya makazi na umiliki wa
rasilimali katika ngazi ya kaya.
Dkt. Mpango alisema
kuwa Utafiti huo utaiwezesha Serikali kupima kiwango
cha hali ya umaskini wa kipato, chakula na pengo baina ya matajiri na maskini kuanzia
kipindi cha mwaka 2013 hadi sasa.
“Takwimu zilizopo hivi sasa zinaonesha kwamba kiwango cha umasikini wa
kipato ulipungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 28.2 mwaka
2012” Alisema Dkt. Mpango.
Alisema pamoja na takwimu hizo, bado kiwango cha umasikini ni kikubwa
na kwamba Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali
inahakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za msingi za kijamii kwa kadri
uchumi unavyokua hivyo kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la umasikini.
“Nimefurahi kuelezwa kuwa utafiti huu utakusanya takwimu katika kaya
binafsi 10,460 kwa Tanzania Bara kuanzia Novemba 2017 hadi Novemba 2018 na
kwamba kupitia zoezi hili, Serikali ya Awamu ya Tano imetoa ajira kwa vijana
wapata 620 katika maeneo ya vijijini na mijini” alieleza Dkt. Mpango.
Aliwaasa wadadisi hao kufanyakazi zao kwa umakini na weredi mkubwa ili
takwimu zitakazopatikana ziwe sahihi na kuonya kuwa Serikali haitasita
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaojaribu kuvuruga zoezi hili.
Awali, Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa alieleza kuwa ukusanyaji wa
Takwimu za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi utafanyika katika
maeneo 754 yaliyochaguliwa kitaalamu kwa kutumia takwimu za Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012.
“Utafiti huu utakuwa wa
saba tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961, ambapo tafuti nyngine
zilifanyika 1969, 1991/92, 2001, 20117 na mwaka 2011/12” aliongeza Dkt. Chuwa.
Alisema kuwa utafiti
huo mpya utafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ijulikanayo kama Survey
Solution (CAPI) na kwamba matokeo ya awali ya utafiti huo yanatarajiwa kutolewa
ndani ya miezi sita ijayo ili nchi iweze kufahamu kiwango cha umasikini uliopo
katika jamii hivi sasa baada ya kufanyika kwa utafiti kama huo miaka mitano
iliyopita.
“Utafiti wa mwisho
uliofanyika mwaka 2011/2012 uliotumia karatasi uligharimu shilingi bilioni 20 lakini
kwa kutumia teknolojia mpya, utafiti huu utagharimu kiasi cha shilingi bilioni
10 pekee” alisisitiza Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa alisema
kuwa anaamini matokeo ya utafiti huo yatakuwa chachu ya kupata takwimu za
msingi kwa ajili ya kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa program mbalimbali
za kitaifa na kimataifa zenye kulenga kupunguza kiwango cha umasikini nchini.
Naye Mkurugenzi
Msaidizi Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu ya TEHAMA Bw.
Baltazar Kibola alisema kuwa watatoa ushirikiano wakutosha kwa wadadisi hao
katika ngazi zote kuanzia Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Vijiji na Vitongoji
ikiwemo kufanyia marekebisho vitendeakazi vya kukusanyia takwimu hizo vikipata
hitililafu ili azma ya Serikali ya kupata takwimu sahihi itimie kama
ilivyopangwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni