Gerald
Deus (30), mkazi wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita aliyetoka
jela kwa msamaha wa Rais, amehukumiwa tena kifungo cha miaka 15 jela.
Deus
aliyehukumiwa kifungo hicho juzi na Mahakama ya Mwanzo Bukombe baada ya
kukiri kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu, ni miongoni mwa wafungwa
8,157 waliopewa msamaha Desemba 9 na Rais John Magufuli.
Msamaha huo wa Rais ulitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).
Deus
alihukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Bukombe, Damas
Gakwaya baada ya kukiri kosa la kupora Sh300,000 kutoka kwa Dina Mwende,
mfanyabiashara wa soda za jumla wilayani Bukombe.
Tukio
hilo kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Polisi, Mohamed Simai
lilitokea katika Mtaa wa Malendeja, Kata ya Katente wilayani Bukombe saa
sita mchana Desemba 14, ikiwa ni siku nne tu tangu mshtakiwa huyo atoke
gerezani.
Simai
aliiambia Mahakama kuwa kabla ya kupora kiasi hicho cha fedha,
mshtakiwa alifika dukani akijifanya anataka kununua soda za jumla kwa
ajili ya vibarua aliodai walikuwa wakilima shambani kwake.
“Wakati
muuza soda akiendelea kupanga kreti dukani, ghafla mshtakiwa alimvamia
na kumpora Sh300,000 na kuanza kutimua mbio kabla ya kukamatwa na raia
wema waliojitokeza kutoa msaada baada ya kelele za aliyeporwa fedha,”
Simai aliieleza Mahakama.
Mwendesha
mashtaka alisema baada ya kumkamata, wananchi walianza kumshambulia
lakini aliokolewa na polisi waliofika eneo la tukio. Baada ya kusomewa
mashtaka, mshtakiwa Deus alikiri kutenda kosa hilo na kuiomba Mahakama
imhurumie kwa kumpa adhabu ndogo kwa sababu ana siku tano tu tangu
alipotoka gerezani kwa msamaha wa Rais Magufuli.
Akitoa
hoja baada ya mshtakiwa kukiri kosa, mwendesha mashtaka aliiomba
Mahakama kumpa Deus adhabu kali kwa sababu anaonekana ni mhalifu mzoefu
na hajajifunza kwa kipindi cha miezi sita aliyokaa gerezani akitumikia
kifungo cha mwaka mmoja alichohukumiwa kwa kosa la wizi.
Kwa
mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Juni Mosi, mwaka huu, Deus
alihukumiwa kifungo cha miezi 12 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa
la wizi wa nguo mali ya Naomi Musa, mkazi wa Mtaa wa Kapela, Kata ya
Igulwa katika mji mdogo wa Ushirombo wilayani Bukombe.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mujuni Mchunguzi wa Mahakama ya Mwanzo Bukombe katika shauri la jinai namba 188/2017.
Kabla
ya kutoka kwa msamaha wa Rais Desemba 9, mshtakiwa alikuwa akitumikia
adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela katika Gereza la Kahama ambako
ndiko alikorejeshwa juzi.
“Kwa
sababu mshtakiwa amekiri kosa; na kwa kuzingatia ametenda kosa hilo
siku chache tu baada ya kutoka Magereza kwa msamaha wa Rais; naiomba
Mahakama kumpa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye
nia ya kutenda kosa kama hilo,” aliomba Simai.
Akitoa
hukumu, Hakimu Gakwaya aliyeonyesha mshangao kwa mshtakiwa kushindwa
kutumia vizuri msamaha wa Rais Magufuli, alisema Mahakama inamhukumu
kifungo cha miaka 15 jela badala ya miaka 30 aliyostahili kwa mujibu wa
sheria kwa sababu hakuisumbua Mahakama kwa kukiri kosa.
“Kwa
sababu hujaisumbua Mahakama kwa kukiri kosa; nakupa adhabu ya onyo ya
miaka 15 na kazi ngumu gerezani ili iwe fundisho kwako na kwa wengine,”
alisema hakimu Gakwaya.
Adhabu
hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 285 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa
ya Jinai sura ya 16 na marekebisho yake ya mwaka 2002.
Post a Comment
karibu kwa maoni