Watu
wawili wameuawa wilayani Kalambo mkoani Rukwa katika matukio tofauti,
likiwamo la mtoto kuuawa kwa kupigwa ngumi na mateke tumboni na baba
yake.
Katika
tukio la kwanza lililotokea Januari 1 saa 4 usiku, mtoto Benedicto
Salumu (13), mkazi wa Kitongoji cha Saint Maria Kata ya Matai wilayani
humo, inadaiwa alipigwa na baba yake hadi kufa baada ya ugomvi kuzuka
kati ya mama na baba wa mtoto huyo.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Rafael Sinyangwe, kwa muda
mrefu kumekuwapo ugomvi baina ya baba wa mtoto, Pius Salum (46) na
mkewe, Hilda Mpangamila (37), akimtuhumu mkewe kuwa mtoto huyo si wa
kwake.
Mwenyekiti
huyo alisema Salum mara kadhaa amekuwa akiwalalamikia ndugu zake kuwa
mkewe alibeba ujauzito wa mtoto huyo wakati akiwa amekwenda kutafuta
maisha na aliporudi alihisi mkewe ni mjamzito.
Sinyangwe aliongeza kuwa tofauti hizo zilisababisha mvutano mkubwa wa mara kwa mara kati ya wanandoa hao.
Mwenyekiti
Sinyangwe alidai siku ya tukio hilo mtuhumiwa akiwa ametoka
kusherehekea Mwaka Mpya, aliingia chumbani na kukuta mtoto huyo akiwa
amelala kisha kuanza kumpiga na ngumi na mateke sehemu mbalimbali za
mwili wake ikiwamo tumboni hadi kusababisha kifo chake.
Aliendelea
kudai kuwa baada ya kumua, alimpiga pia mke wake akidai amemsababishia
kulea mtoto asiyekuwa wake kwa muda mrefu, hali mbayo ilikuwa ikimuudhi
na kumkosesha amani.
Katika
tukio jingine lililotokea Januari 1 majira ya jioni, mkazi wa Kijiji
cha Kafukoka kata ya Kisumba wilayani Kalambo mkoani Rukwa Kalasto
Katanti (40) aliuawa na ndugu zake baada ya kipigo kikali wakidai
kuchukizwa na madeni aliyonayo.
Kabla
ya kuuawa kwa kipigo Katanti alikuwa anadaiwa shilingi 64,000, deni
ambalo lilikuwa ni la muda mrefu kiasi ambacho alionekana ameshindwa
kulilipa.
Katibu
Tawala wa wilaya hiyo, Frank Sichalwe, alisema ndugu zake wawili ambao
ni Florens Zunda (38) na Dafusi Zunda (35) ndipo walipoamua kumpiga hadi
kumuua wakidai wamechoshwa na tabia yake ya kukopa fedha wakati anajua
hana uwezo wa kulipa, kitendo kinachodhalilisha ukoo wao.
Kamanda
wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa mauaji
hayo na Kuongeza kuwa watuhumiwa wanashikiliwa na polisi na
watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.
Post a Comment
karibu kwa maoni