
Akizungumza
na waandishi wa habari nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam
jana, Mbowe alisema licha ya kutambua kuwa mwaka 2017 ulikuwa mgumu kwa
vyama vya upinzani, mwaka huu watahakikisha wanapambana ili kurudisha
mchakato wa Katiba mpya.
“Jambo kubwa tunalopigania hapa ni kuwa na tume huru ya uchaguzi,” alisema.
Moja
ya mambo yanayolalamikiwa kuwa chombo hicho hakina uhuru ni uteuzi wa
viongozi wake kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, na muundo wake.
Kwa
sasa, NEC ina wafanyakazi wa ofisi ya makao makuu tu, wakati katika
ngazi za wilaya ambako uchaguzi huratibiwa, inategemea wakurugenzi wa
halmashauri ambao pia ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa chombo
hicho.|
Katika
mkutano wa jana, Mbowe alisema suala la ukosefu wa fedha ili kuendelea
na mchakato huo halina mashiko kwa kuwa kinachohitajika ni dhamira ya
dhati.
“Tumeshatumia
fedha nyingi hadi kufikia mchakato wa Katiba mpya ulipoishia,
kinachohitajika ni dhamira ya dhati ya kupata Katiba Mpya. Rais
anatakiwa kutambua kuwa Katiba ni matakwa ya wananchi si mapenzi ya
Rais,” alisema.
Aliwataka wadau kutoviachia vyama vya siasa pekee kudai Katiba mpya kwa kuwa ina manufaa kwa Watanzania wote.
Mbowe alisema watahakikisha wanatumia kila aina ya mbinu ili kufanikisha kuendelea na mchakato huo.
“Leo
tunamaliza mwaka 2017 lakini kwetu ulikuwa mgumu kushinda yote tangu
nchi iingie katika demokrasia ya vyama vingi miaka 25 iliyopita,”
alisema.
Alisema licha ya kuijenga demokrasia kwa kipindi chote hicho, utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano umerudisha nyuma.
“Pamoja na kuwa mimi ni mwenyekiti wa Chadema siwezi kuitisha mkutano wa wanachama hapa Dar es Salaam,” alisema.
Mchakato
wa Katiba Mpya ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka
2011 alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph
Warioba.
Hata
hivyo, mchakato huo uliishia kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo
licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambayo haijapigiwa kura ya
maoni hadi leo, baadhi ya vyama vya upinzani vilijitoa na kuunda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kikiwemo Chadema na kupinga mchakato huo
kwa maelezo kuwa ulivurugwa na chama tawala.
Vyama
vya upinzani vimejikuta katika wakati mgumu tangu kuingia madarakani
Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na kushindwa kufanya mikutano ya
hadhara, viongozi wake kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi, kufanya fujo
na uharibifu.
Mbowe alisema wakati vyama vya upinzani vinakatazwa kufanya mikutano, chama tawala kinafanya.
“Hakuna
usawa katika kufanya siasa, ni sawa na kumfunga mikono bondia halafu
unataka apigane na mwenzake ambaye hajafungwa mikono,” alisema.
Mbowe
alisema kama Serikali inaona hakuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa vyama
vingi vya siasa ni bora vikafutwa kuliko kuvizuia visifanye siasa.
Post a Comment
karibu kwa maoni