0
 Jeshi la polisi mkoani Morogoro linamsaka mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mwita Marwa (30) kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga mpenzi wake Kibua Adam (39) baada ya kutokea kutokuelewana kati yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema tukio hilo lilitokea Januari 22 mwaka huu katika eneo la Modeco Manispaa ya Morogoro ambapo mwanafunzi huyo alitoweka baada ya tukio hilo.

Amesema siku ya tukio mwanafunzi huyo na mpenzi wake ambaye ni mhudumu wa baa walichukua chumba katika nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kama Aluta ambapo walilala lakini baadaye mwili wa marehemu ulikutwa chumbani.

“Dada huyu mkazi wa Kihonda alikutwa ameachwa chumbani akiwa ameshafariki na baada ya uchunguzi ilionekana kwamba marehemu alinyongwa shingo kabla ya kifo chake,” amesema Kamanda Matei.

Hata hivyo, kamanda huyo amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alimwandikia ujumbe wa simu dada wa marehemu aitwaye Happiness Adamu ujumbe akisema kwamba tayari marehemu keshatangulia na yeye mtuhumiwa atafuata.

“Nasikitika sana hamtatuona hapa duniani Mwita na Kibua, mimi ninayeandika meseji hii ni Mwita, nikimaliza nakunywa sumu au vidonge nife na mimi nimechoka na dunia na Kibua yeye keshatangulia, njooni hapa Aluta Bar mtutoe chumbani tulipolala,” ulisomeka ujumbe huo.

Hata hivyo, watu wa karibu wa marehemu ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema marehemu alikuwa na mpenzi mwingine kabla ya Mwita na walipokorofishana ndipo alipoamua kuwa na Mwita lakini siku chache kabla ya tukio alimwambia Mwita kwamba mpenzi wake wa awali amejirekebisha hivyo anataka kurejeana naye jambo ambalo mtuhumiwa alikuwa analipinga.

Kamanda Matei amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Morogoro na jeshi hilo bado linaendelea na jitihada za kumsaka mtuhumiwa.   

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top